Jul 25, 2016 07:56 UTC
  • Shambulizi jingine la bomu Iraq, makumi wauawa

Kwa akali watu 18 wameuawa na wengine 23 kujeruhiwa katika hujuma nyingine ya kigaidi mashariki mwa Iraq, siku moja baada ya shambulizi jingine la bomu kuua na kujeruhi makumi ya watu katika mji mkuu Baghdad.

Habari zinasema kuwa, shambulizi hilo la bomu limefanyika katika mji wa al-Khalis, yapata kilomita 15 kaskazini mashariki mwa mji wa Baqubah, makao makuu ya mkoa wa Diyala. Omar Maan al-Korawi, Mkuu wa Baraza la mkoa huo amesema gari lililokuwa na mada za mirupuko liliingia katika jengo la Idara ya Kilimo mjini hapo na muda mfupi likaripuka na kusababisha maafa hayo.

Maafisa Usalama wa Iraq katika kituo cha upekuzi mjini Baghdad baada ya shambulizi la kigaidi Julai 25

 

Haya yanajiri siku moja baada ya watu zaidi ya 12 kupoteza maisha na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulizi la bomu lililotokea mapema jana katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Mshambuliaji wa kujitolea muhanga alijiripua katika kituo cha upekuzi kilichoko katika wilaya ya Kadhimiya, kaskazini mwa Baghdad na kusababisha maafa na majeraha hayo.

Hujuma ya kigaidi katika mtaa wa Karrad mjini Baghdad Julai 3 ilikuwa mbaya zaidi nchini Iraq tokea uvamizi wa Marekani nchini humo miaka 13 iliyopita, ambapo watu zaidi ya 300 waliuawa.

Tags