Wananchi wa Uturuki waandamana kulaani jinai za Israel Gaza
Maelfu ya wananchi wa Uturuki wameandamana katika mji muhimu wa nchi hiyo Istanbul na kutangazza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza.
Waandamanaji hao, wakiwa wamebeba mabango na maberamu, wamepiga nara za kulaani jinai za utawala wa Kizayuni pamoja na washirika wake na kutoa mwito kwa jami ya kimataifa kuchukua hatua za kukomesha jinai za Israel huko Gaza.
Maandamano haya makubwa yalianza jana (Jumapili) baada ya Swala ya adhuhuri na yalikuwa na kauli mbiu "Ulinzi wa Gaza" kutoka Msikiti maarufu wa Pasha huko Istanbul na kuendelea hadi Hifadhi ya Kitaifa ya Pasha.
Maandamano hayo yamefanyika kwa ajili ya kusisitiza mshikamano na wananchi na Gaza na muqawama wake dhidi ya utawala wa Kizayuni na kujadidisha baiya kwa mashahidi waliojitolea mhanga kwa ajili ya Palestina.
Waandamanaji hao wameitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati haraka iwezekanavyo ili kuokoa maisha ya watu wasio na hatia na kutuma misaada ya kibinadamu huko Gaza. Kadhalika wametoa mwito wa kuwafungulia mashitaka viongozi wa utawala wa Kizayuni kwa kutekeleza jinai ya mauaji ya kimbari katika eneo hili.