UN yaonya kuhusu hatari ya kuenea mapigano kaskazini mashariki mwa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120536-un_yaonya_kuhusu_hatari_ya_kuenea_mapigano_kaskazini_mashariki_mwa_syria
Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria ameonya kuhusu kuenea migogoro na mapigano, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo baada ya kupinduliwa serikali ya Rais Bashar al Assad.
(last modified 2024-12-24T03:20:00+00:00 )
Dec 24, 2024 03:20 UTC
  • UN yaonya kuhusu hatari ya kuenea mapigano kaskazini mashariki mwa Syria

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria ameonya kuhusu kuenea migogoro na mapigano, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo baada ya kupinduliwa serikali ya Rais Bashar al Assad.

Kuongezeka uwezekano wa magaidi wa Daesh (ISIS) kurejea madarakani na misimamo mikali ya Uturuki dhidi ya Wakurdi kumeiweka Syria katika hatari ya kukumbwa na mgogoro mkubwa zaidi kuliko hapo awali.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Geir Otto Pedersen, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Syria akielezea wasiwasi wake kuhusu hatari za kuenea migogoro kaskazini mashariki mwa Syria.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, mgogoro kati ya Wakurdi wa Syria na makundi yanayoungwa mkono na Uturuki unapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.

Pedersen ameongeza kuwa, utatuzi wa tofauti hizo unapaswa kufanywa katika wakati huu ambapho Syria iko kipindi nyeti na muhimu mno cha mpito na kuingia madarakani watawala wapya.

Mwakilishi huyo maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amedai kuwa, "Ahmed al-Shara" maarufu kwa jina la "Abu Mohammad al-Jolani" aliyeongoza vikosi vya upinzani vyenye silaha vilivyompindua Rais Bashar al Assad ameahidi kutafuta suluhisho ambalo litajumuisha makundi yote ya Syria.

Kuanzia Novemba 27, 2024, magaidi na wapinzani nchini Syria, wakiungwa mkono na baadhi ya nchi, walianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Syria katika mikoa tofauti ya nchi hiyo, na hatimae kupelekea kuanguka serikali ya Rais Bashar al-Assad tarehe 8 Disemba 2024.