Ansarullah yatangaza kukamatwa maajenti wa Mossad na CIA nchini Yemen
Harakati ya Ansarullah ya Yemen imeitangaza kwamba imekamata idadi kadhaa ya "majasusi waliokuwa wakifanya kazi kwa maslahi ya shirika la ujasusi la Israel, Mossad, na shirika la ujasusi la Marekani, CIA."
Taarifa iliyotolewa na Ansarullah imesema "vitengo vya usalama vimefanikiwa, katika siku zilizopita, kukamata idadi (ambayo haikutajwa) ya majasusi, ambao walishawishiwa na kuajiriwa na jasusi anayesakwa, Hamid Hussein Fayed Majli."
Taarifa hiyo imeeleza kwamba "majasusi hawa walipewa kazi kadhaa, hasa kufuatilia na kukusanya taarifa kuhusu wataalamu, maabara, majukwaa, viwanda na mitambo ya kurushia makombora na ndege zisizo na rubani zinazotumiwa kumshambulia adui Mzayuni, na vile taarifa za maeneo na kambi za vikosi vya majini na maghala ya silaha."
Imeongeza kuwa: "Kazi za majasusi hao pia ni pamoja na kufuatilia na kukusanya taarifa kuhusu mahali alipo kiongozi wa Ansarullah, Abdul-Malik al-Houthi, na baadhi ya viongozi wa kisiasa, kijeshi na masuala ya usalama wa Yemen, na watu mashuhuri katika masuala ya kijamii wanaopinga Israel na Marekani."
Ansarullah imesema: "Majasusi hawa pia walipewa kazi ya kujaribu kupenya, kuajiri, na kupandikiza vibaraka katika safu za vikosi vya jeshi ulinzi na usalama la Yemen.
Taarifa hiyo imeonya kuhusu hatari ya kufanya kazi kwa maslahi ya mashirika ya kijasusi ya Marekani na Israel, ambako adhabu yake inaweza kuwa kifo.
Wananchi wa Yemen wametangaza uungaji mkono wao wa wazi kwa mapambano ya Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel tangu utawala huo ghasibu ulipoanzisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023.