Wanajeshi 40 wa Israel waangamizwa kaskazini mwa Gaza
Makundi ya muqawama ya Wapalestina yanaendelea na operesheni zao dhidi ya jeshi katili la Israel kwa kuvurumisha makombora zaidi kwenye ngome za utawala wa Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Redio ya Jeshi la Israel jana Jumapili ilikiri kuwa wanajeshi 40 Waisraeli wameuawa kaskazini mwa Gaza katika mapambano na Wapalestina tangu kuanza kwa mashambulizi ya kijeshi ya utawala huo mjini Jabalia mwezi Oktoba.
Ripoti hiyo aidha imesema wanajeshi 5,541 wa Israel wamejeruhiwa katika kipindi hiki. Jeshi la Israel kwa kawaida linakabiliwa na tuhuma za kuficha idadi kubwa ya vifo vya wanajeshi wake ili wengine wasiogope kwenda vitani.
Kulingana na takwimu za jeshi, idadi ya askari wake walioangamizwa tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza, Oktoba 7, 2023, sasa imeongezeka hadi wanajeshi 824.
Takwimu hizo zinajumuisha wanajeshi waliouawa katika Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, Lebanon na ndani ya Israel.
Wapigania ukombozi wa Palestina wanasisitiza kwamba hasara ya vikosi vya utawala haramu wa Israel ni kubwa zaidi kuliko inayotangazwa.