Hizbullah ya Lebanon yamshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120824-hizbullah_ya_lebanon_yamshukuru_kiongozi_muadhamu_wa_mapinduzi_ya_kiislamu
Naibu Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Hizbullah ya nchini Lebanon amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kwa jinsi anavyoyapa umuhimu mkubwa masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu yakiwemo wa Lebanon.
(last modified 2024-12-30T23:24:36+00:00 )
Dec 30, 2024 23:24 UTC
  • Hizbullah ya Lebanon yamshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Naibu Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Hizbullah ya nchini Lebanon amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, kwa jinsi anavyoyapa umuhimu mkubwa masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu yakiwemo wa Lebanon.

Katika shukrani zake hizo, Sheikh Ali Damush amesema kuwa, tunaishukuru Iran, Iraq na nchi zenye nia njema ya kusaidia kuijenga upya Lebanon.

"Wale wote waliofikiri kwamba Hizbullah ya Lebanon haitawalipa fidia wahanga wa mashambulizi ya kikatili ya Israel, wamekatishwa tamaa," ameendelea kusema Sheikh Damush na kuongeza kuwa: "Watu hawa walifurahia dhana zao kwamba Hizbullah haina uwezo wa kufidia uharibifu wa watu wake, lakini chama hiki kimeinuka kutoka kwenye vifusi ili kuponya majeraha ya watu wake."

Ameendelea kusema kwamba, tutajenga upya magofu kwa baraka ya damu ya mashahidi na mikono yenye nguvu ya wanamapambano wetu.

Sheikh Damush amekumbusha kuwa kipaumbele katika ujenzi huo ni kwa familia ambazo nyumba zao zimeharibiwa kikamilifu au zimeharibiwa kidogo, hasa katika vijiji vya mpakani, ili waweze kurejea katika makazi yao haraka iwezekanavyo.

Aidha amesema kwamba, kwa kuwa Muqawama umeshinda na ummemlazimisha adui mvamizi kuomba usitishaji vita, ni hivyo hivyo ujenzi huo mpya pia utashinda uharibifu uliofanywa na Israel.

Ameongeza kuwa, Hizbullah imenyanyuka kutoka kwenye magofu ya vita vya uharibifu ili kuwathibitishia Walebanon na walimwengu kwamba ahadi yake ilikuwa ya kweli.