Rais wa Algeria: Katu hatutaiacha mkono Palestina
Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune amesisitiza kuwa, nchi yake katu haitaiacha mkono Palestina na kwamba, itaendelea kuliunga mkono taifa hilo madhlumu.
Akihutubia Bunge, Rais wa Algeria amesisitiza kuwa: "Tutaendelea kuunga mkono taifa la Palestina sambamba na mapambano yao ya kufikia haki zao halali."
Sambamba na kusisitiza kuwa Algeria itasimama upande wa Palestina na watu wote wanaodhulumiwa duniani, Rais Tebboune alisema: Tangu Algeria ilipokubaliwa uanachama wake usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, iliingia katika vita kwa ajili ya Palestina.
Ikumbukwe kuwa, Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune amewahi kutangaza kuwa jeshi la nchi yake liko tayari kupeleka wanajeshi katika Ukanda wa Gaza kuwasaidia Wapalestina wa eneo hilo punde tu mipaka kati ya Misri na Ukanda wa Gaza itakapofunguliwa.
Rais wa Algeria ameeleza mara kadhaa uungaji mkono kamili wa nchi yake kwa kadhia ya Palestina na kusisitiza kuwa, ukombozi wa Palestina ni kadhia tukufu.
Mwishoni mwa mwaka uliopita pia, Wizara ya Utamaduni na Sanaa ya Algeria ilitangaza kuakhirishwa shughuli zote za kitamaduni na matamasha kote nchini humo, ikiwa ni pamoja na Tamasha la Filamu la Annaba la Mediterania ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika Novemba 3 hadi 9 mwaka jana kama ishara ya kuunga mkono kadhia ya Palestina na kulalamikia jinai za Israel.