Ghaza yaanza Mwaka Mpya kwa kushambuliwa kikatili na Israel
Katika dakika za awali kabisa za kuingia Mwaka Mpya wa 2025, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limefanya mashambulizi mengine ya kinyama kwenye Ukanda wa Ghaza kutoka kaskazini hadi kusini mwa ukanda huo uliozingirwa kila upande.
Mapema leo Jumatano alfajiri ambayo ni siku ya kwanza ya Mwaka Mpya wa 2025, duru za ndani ya Palestina zimeripoti habari ya kutokea mashambulizi ya kijinai ya utawala wa Kizayuni kuanzia kaskazini hadi kusini mwa Ukanda wa Ghaza.
Taarifa ya vyombo hivyo vya habari vya Palestina imesema: "Mizinga ya jeshi la Israel imeshambulia eneo la mashariki mwa mji wa Khan Yunis na pia magharibi mwa mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza."
Jeshi la Israel linaloikalia kwa mabavu Quds limeendelea pia kuripua majengo ya raia wa Palestina, kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.
Vilevile Wapalestina kadhaa wameuawa shahidi na kujeruhiwa wakati wanajeshi makatili wa Israel waliposhambulia jengo la makazi ya raia katika kambi ya wakimbizi ya El Brij ya katikati mwa Ukanda wa Ghaza.
Ripoti hiyo pia imesema: "Wapalestina kadhaa wamejeruhiwa kutokana na mashambulio yaliyofanywa na Israel kwenye makazi ya watu katika mji wa Jabalia wa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza."
Kwa upande wake, televisheni ya Al Jazeera imeripoti kwamba, nyumba ya Rami Abu Taymeh, ripota wa televisheni hiyo nayo imeshambuliwa kikatili na utawala wa Kizayuni katika eneo la al-Bukhari la Mji wa Ghaza na kupelekea kujeruhiwa watu wa familia yake.