Wairani wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 5 ya kuuawa shahidi Jenerali Soleimani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120952-wairani_wanaadhimisha_kumbukumbu_ya_miaka_5_ya_kuuawa_shahidi_jenerali_soleimani
Leo Ijumaa katika mji aliozaliwa na eneo la kaburi la Jenerali Soleimani, kumeshuhudiwa mafuriko ya maashiqi na wapenzi wa kamanda huyo mashuhuri huku kukiwa na baridi kali na theluji wakati huu wa kumbukumbu ya miaka mitano ya kuuawa kwake shahidi.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jan 03, 2025 04:06 UTC
  • Wairani wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 5 ya kuuawa shahidi Jenerali Soleimani

Leo Ijumaa katika mji aliozaliwa na eneo la kaburi la Jenerali Soleimani, kumeshuhudiwa mafuriko ya maashiqi na wapenzi wa kamanda huyo mashuhuri huku kukiwa na baridi kali na theluji wakati huu wa kumbukumbu ya miaka mitano ya kuuawa kwake shahidi.

Katika miji mingine ya Iran, ukiwemo mji mkuu, Tehran, katika kipindi cha siku tatu kumefanyika  mijumuiko mbalimbali ya kumkumbuka Shahidi Jenerali Soleimani.

Akizungumza Jumatano katika hafla ya kumuenzi kamanda huyo shujaa, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisifu na kukutaja kuwa ni kwa kipekee kujitolea kwa kamanda mkuu wa Iran wa kupambana na ugaidi, Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Naye Rais Rais Massoud Pezeshkian akizungumza Alhamisi amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea na njia iliyoanzishwa na kamanda shujaa wa kupambana na ugaidi, Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kwa nguvu zake zote.

Jenerali Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) na Abu Mahdi al-Muhandis, mkuu wa Kitengo cha Uhamasishaji cha Iraq (Hashdu Shaabi) na wanamapambano wenzao waliuawa shahidi katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani Januari 3, 2020 karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. Shambulizi hilo la kigaidi liliidhinishwa na Rais wa wakati huo wa Marekani, Donald Trump.

Makamanda hao wawili walikuwa wakiheshimika sana katika eneo la Asia Magharibi na duniani kote kwa sababu ya jukumu lao muhimu katika kupambana na kundi la kigaidi la Daesh katika eneo hilo hususan Iraq na Syria.

Katika muda wa chini ya wiki moja baada ya shambulio hilo, wabunge wa Iraq waliidhinisha muswada ulioitaka serikali kuwafukuza wanajeshi wote wa kigeni wanaoongozwa na Marekani nchini humo.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pia lilitwanga kambi ya Marekani ya Ain al-Asad katika mkoa wa magharibi wa Anbar nchini Iraq kulipiza kisasi mauaji ya Jenerali Soleimani.