Wapalestina wengine 49 wauawa shahidi Gaza
Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, raia wasiopungua 49 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya Wazayuni katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza kuanzia Jumanne asubuhi hadi jana usiku.
Duru za habari zinaripoti kuwa, jana (Jumanne), jeshi la Israel kwa mara nyingine tena lililenga na kushambulia maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza.
Raia wasiopungua 8 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya kulipuliwa kwa kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza huko Palestina.
Katika shambulio hilo katika eneo la al-Mawasi katikati mwa Gaza, ambalo limetangazwa kuwa eneo salama na Wazayuni, idadi kadhaa ya raia waliuawa shahidi, na majina ya watoto 4 yanaonekana miongoni mwa mashahidi.
Vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Ghaza tangu Oktoba 7, 2023, hadi sasa yamepelekea Wapalestina karibu 46,00 kuuawa shahidi na wengine 109,064 kujeruhiwa.
Wizara ya Afya ya Palestina imeeleza kuwa, zaidi ya wafanyakazi 300 wa sekta ya afya, 35 wa vikosi vya ulinzi wa raia na wafanyakazi 135 wa Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) wameuawa shahidi katika hujuma inayoendelea ya utawala ghasibu wa Israel.
Uungaji mkono wa wazi wa Marekani na nchi za Magharibi umepelekea kushuhudiwa faili jeusi la viongozi watenda jinai wa utawala wa Kizayuni wanaoua watu wasio na ulinzi wala hatia. Bila shaka wale wote wanaohami na kuunga mkono jinai za Israel wanahusika pia katika jinai na mauaji ya kimbari ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.