HAMAS: Vitisho vya Trump havitutii hofu yoyote
Jan 11, 2025 00:09 UTC
Mjumbe wa ngazi ya juu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema: "Vitisho vya Marekani havina umuhimu wowote kwa wananchi wa Palestina. Wapalestina wanajua kwamba wako kwenye haki na wanapigania haki na malengo yao matakatifu ili waweze kuishi katika nchi yao wenyewe kama walivyo watu wa mataifa mengine duniani".
Abdul Rahman Shadid, mjumbe wa ngazi ya juu wa harakati ya Hamas ametoa mjibizo kwa kitisho cha rais Mteule wa Marekani Donald Trump aliyetamka kwamba milango ya moto itafunguka iwapo mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Ghaza hawataachiwa huru na akasema: Marekani imemuunga mkono kikamilifu na kwa kila hali adui Mzayuni katika vita vya kiwendawazimu na mauaji ya kimbari anayofanya dhidi ya wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza kwa muda wa miezi 15 iliyopita.
Abdul Rahman Shadid ameongeza kuwa: Serikali ya Marekani, bila kujali kama ni ya Democrats au Republicans, ni mshirika halisi katika vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na utawala wa Kizayuni, ambavyo vinawalenga watoto, wanawake, wazee, nyumba, waandishi wa habari, wafanyakazi wa sekta ya tiba, skuli na vyuo vikuu.
Halikadhalika, mjumbe huyo mwandamizi wa Hamas amesema: "Tunaamini kuwa vitisho kama hivi vinavyotolewa na Marekani ni ithibati ya ubabe na uonevu, upindukiaji mipaka na utumiaji sera za kuuma na kupuliza unaofanywa na Washington; na badala ya kutoa vitisho, inachopaswa kufanya serikali ya Marekani na Trump ni kusimama pamoja na wananchi wa Palestina kwa dhulma wanazofanyiwa ambapo kwa muda wa miaka 76 wamekuwa wakiteseka kutokana na uvamizi wa kifashisti na utendaji jinai.
Abdul Rahman Shadid amekumbusha kuwa, mashine ya moto wa vita ya jeshi la utawala wa Kizayuni inayoendeshwa kwa uungaji mkono kamili wa Marekani, haijabakisha chochote katika Ukanda wa Ghaza bali imeliangamiza eneo hilo na akasisitiza kwa kusema: "Vitisho vya Marekani havina umuhimu wowote kwa wananchi wa Palestina. Wapalestina wanajua kwamba wako kwenye haki na wanapigania haki na malengo yao matakatifu ili waweze kuishi katika nchi yao wenyewe kama walivyo watu wa mataifa mengine duniani".../
Tags