Kulazimishwa utawala wa Kizayuni kuondoka kabisa kusini mwa Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121670-kulazimishwa_utawala_wa_kizayuni_kuondoka_kabisa_kusini_mwa_lebanon
Kufuatia ziara ya Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa nchini Lebanon, António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amezuru nchi hiyo na kulitaka jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuondoka kabisa katika maeneo linayoyakalia kwa mabavu kusini mwa Lebanon.
(last modified 2025-01-20T04:34:09+00:00 )
Jan 20, 2025 04:34 UTC
  • Kulazimishwa utawala wa Kizayuni kuondoka kabisa kusini mwa Lebanon

Kufuatia ziara ya Emmanuel Macron, Rais wa Ufaransa nchini Lebanon, António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amezuru nchi hiyo na kulitaka jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuondoka kabisa katika maeneo linayoyakalia kwa mabavu kusini mwa Lebanon.

António Guterres, baada ya kukutana maafisa wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) huko Beirut, amekutana na maafisa mbalimbali wa Lebanon na kujadiliana nao kuhusu kudumishwa usitishaji mapigano, utekelezaji kamili wa makubaliano ya usitishaji mapigano, na pia Azimio la 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pia ametembelea makao makuu ya vikosi vya Umoja wa Mataifa huko Naqoura, kusini mwa Lebanon, ambapo amewaambia wanajeshi wa UNIFIL kwamba: "Ninyi siyo tu mko kwenye mstari wa bluu wa Lebanon, bali pia mpo kwenye mstari wa mapambano kwa ajili ya amani." Alisisitiza kuwa uwepo wa jeshi la Israel katika eneo la operesheni za UNIFIL na kufanya operesheni za kijeshi ndani ya ardhi ya Lebanon ni ukiukaji wa Azimio 1701 na ni tishio la kudumu kwa usalama wa askari hao, jambo ambalo lazima likomeshwe mara moja.

Katika mkutano wake na Youssef Aoun, Rais wa Lebanon, Guterres ametangaza utayari wa kutumika zana zote za jamii ya kimataifa kusaidia Lebanon na kusisitiza kwamba atafanya kila juhudi kuhakikisha vikosi vya Israeli vinaondoka kutoka kusini mwa Lebanon kufikia Januari 27.

Ameongeza: "Kuondoka kwa vikosi vya Israeli na kupelekwa kwa vikosi vya jeshi la Lebanon katika mipaka ya pamoja kutafungua ukurasa mpya wa amani".

Rais wa Lebanon amesema kuwa hatua ya vikosi vya utawala haramu wa Isarel ya kuendeleza operesheni za nchi kavu  na anga, hasa uharibifu wa vijiji vya mpakani licha ya makubaliano ya usitishaji mapigano, ni ukiukaji wa kujitawala Lebanon na matakwa ya jamii ya kimataifa.

Makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Lebanon yalitekelezwa mnamo Novemba 27, 2024, kwa upatanishi wa kimataifa. Hata hivyo, ripoti zinaonyesha kuwa tangu utekelezaji wa makubaliano hayo ya siku 60, vikosi vya anga vya Israel vimefanya mamia ya mashambulizi haramu katika ardhi ya Lebanon.

Magari ya  Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL)

Kwa upande mwingine, Nawaf Salam, Waziri Mkuu wa Lebanon, ambaye ana uzoefu wa kufanya kazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, amesema katika msimamo wake wa kwanza baada ya kushika wadhifa wa Waziri Mkuu kwamba: "Lazima tuishurutishe Israel kuondoka kabisa kutoka eneo la ardhi yetu inayokaliwa kwa mabavu na kuwezesha serikali ya Lebanon kuchukua usimamizi wa maeneo yote ya nchi kama ilivyobainishwa katika Mkataba wa Taif."

Alisisitiza siku ya Ijumaa, katika mkutano wake na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwamba: "Uwepo wa Israel katika ardhi ya Lebanon unaathiri utulivu wa nchi yetu na eneo. Kuondoka kwa Israel hakupaswi kucheleweshwa hata kwa saa moja."

Hizbullah ya Lebanon pia imetoa onyo kwa utawala wa Kizayuni kwamba baada ya kumalizika muda wa usitishaji mapigano, uwepo wowote wa wanajeshi wa utawala huo kama wavamizi katika ardhi ya Lebanon utakabiliwa na hatua kali. Hizbullah pia imetangaza kuwa ikiwa upande mwingine utaheshimu makubaliano ya usitishaji wa mapigano, wao pia watayaheshimu makubaliano hayo. La sivyo, dhima ya matokeo ya uwepo wowote wa wanajeshi wa Kizayuni katika Lebanon itabebwa na Tel Aviv.

Sheikh Naim Qassem, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Jumamosi katika hotuba ya kusherehekea ushindi wa watu wa Gaza na kulazimishwa makubaliano ya usitishaji wa mapigano kwa adui wa Kizayuni, alisema: "Tunamuonya adui wa Kizayuni kwamba asiujaribu uvumilivu wetu. Pia tunaiomba serikali ya Lebanon kuchukua msimamo thabiti dhidi ya uvamizi wa adui na kuonyesha uthabiti katika kukabiliana na ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya usitishaji mapigano unaofanywa na adui wa Kizayuni, ambao umefikia zaidi ya mamia ya mara."