HAMAS: Hali za afya za wafungwa wa Kipalestina zinaakisi 'unyama na ufashisti' wa Israel
Jan 21, 2025 02:34 UTC
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema, hali za kiafya za wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa kutoka kwenye magereza ya Israel zinaakisi "ukatili na ufashisti" wa utawala huo wa Kizayuni.
Utawala wa Kizayuni siku ya Jumapili uliwaachilia huru wafungwa 90 wa Kipalestina, wakiwemo wanawake na watoto, kutoka Gereza la Ofer, magharibi mwa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kwa mujibu wa awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano Ghaza na kubadilishana wafungwa.
Israel ilichukua hatua hiyo baada ya kupita masaa kadhaa tangu Hamas ilipowaachilia huru mateka watatu wanawake wa Kizayuni. Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa wanawake hao watatu wako katika hali nzuri kiafya.
Hamas imeeleza katika taarifa: "picha za mateka watatu wanawake zimeonyesha kuwa wako wazima kiafya kimwili na kisaikolojia, tofauti na wafungwa wetu ambao sura zao zimeonyesha dalili za kupuuzwa na machovu".
Taarifa hiyo ya Hamas imeongezea kwa kusema: "hii inaonyesha wazi tofauti kubwa kati ya maadili na akhlaqi za Muqawama na ukatili na ufashisti wa ughasibu".
Picha, video na taswira za televisheni zimewaonyesha mateka wa Israel walioachiliwa na Hamas wakitabasamu, wakiwa wamevalia nguo safi na nadhifu huku wamebeba "mifuko ya zawadi", kinyume na wanawake Wapalestina walioachiwa kutoka kwenye magereza ya utawala wa Kizayuni ambao wameonekana kwenye nyuso zao kuwa na alama na athari za kupatwa na unyanyasaji na mateso.
Taarifa ya Hamas imeendelea kueleza: "tunawapongeza watu wetu, taifa letu, na watetezi wa uhuru duniani kote kwa kukombolewa kundi la kwanza la wafungwa wetu kutoka kwenye magereza ya utawala ghasibu".
Harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina imesema, taswira za Wapalestina waliokuwa na furaha kubwa huku wakionyesha ishara za ushindi wakati wanawalaki wafungwa wao walioachiliwa huru ni ithibati ya uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa Muqawama na jinsi Muqawama ulivyokita mizizi ndani ya nyoyo zao.
Makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa yalianza kutekelezwa siku ya Jumapili, na hivyo kusitisha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni Israel kwa siku 471 katika Ukanda wa Ghaza.
Makubaliano hayo ya awamu tatu yanajumuisha ubadilishanaji wa mateka kwa wafungwa na kuendeleza utulivu unaolenga kufikiwa mapatano ya kudumu na kuondolewa majeshi ya utawala ghasibu wa Israel huko Ghaza.../
Tags