Vita vya Israel vyaacha mayatima 36,000 na wajane 14,000
Idadi ya watoto wa Kipalestina walioachwa yatima kutokana na vita vya siku 471 vya mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza imefikia zaidi ya 36,000, huku takriban wanawake 14,000 wakibakia baada ya waume zao kuuawa kufuatia hujuma na mashambulio ya kinyama ya Israel katika ukanda huo.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari katika Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza, Zaher Al-Wahidi, amesema kuwa watoto 36,569 wamepoteza mmoja wa wazazi wao na kuwaaacha yatima.
Amesema, takwimu hizo zinaakisi janga la kibinadamu ambalo halijawahi kutokea lililokumba maelfu ya familia za Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Al-Wahidi amesema pia kuwa uvamizi wa Israel "ulisababisha wanawake 13,901 wa Kipalestina kupoteza waume zao na kuwa wajane," kulingana na taarifa alizotoa kwa Shirika la Anadolu.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari katika Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza amesisitiza kwamba,, “takwimu hizi ni ushuhuda wa wazi wa kiwango cha uchungu wa watu wa Gaza, ambao unahitaji kila mtu kufanya kazi ya haraka ili kupunguza mateso ya mayatima na familia zilizoathiriwa na kujenga upya maisha yao katika misingi ya utu wa mwanadamu. ."
Jumatano, Januari 15, 2025, Serikali ya Qatar ilitangaza kupatikana mafanikio ya juhudi za kusimamisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza kati ya pande za Palestina na Israel, na kwamba makubaliano hayo yaliaanza kutekelezwa Jumapili, Januari 19, 2025, ili kuhitimisha miezi zaidi ya 15 ya vita vya kinyama na mauaji ya kimbari ya zaidi ya watu 46,000 yaliyofanywa na jeshi la Kizayuni wa Israel huko Ghaza.