Mateka 200 wa Kipalestina waachiliwa huru; shangwe na furaha zatawala
Wapalestina 200 waliokuwa wakishikiliwa katika magereza ya utawala haramu wa Israel wameachiliwa huru ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya ubadilishanaji mateka baina ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS.
Shirika la Magereza la utawala vamizi wa Israel limetangaza kuwa, mateka 200 wa Kipalestina wameachiliwa huru kama sehemu ya makubaliano ya ubadilishanaji mateka.
Mateka 121 kati ya walioachiliwa huru walikuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na mateka wengine 79 walikuwa wamehukumiwa vifungo vya muda mrefu.
Mateka hao wa Kipalestina wameachiliwa huru baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kuwaachilia huru wanajeshi wa kike wa Kizayuni waliokuwa wakishikiliwa mateka.
Shangwe, nderemo na vifijo vilitawala baada ya Wapalestina hao kuachiliwa huru na kupokewa na familia zao.

Duru za Misri zimeripoti kuwa, mabasi mawili yaliyowabeba wafungwa 70 wa Kipalestina walioachiliwa huru yamewasili Cairo na hao ni wale wafungwa waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela ambapo kwa mujibu wa makubaliano wataendelea na maisha yao nje ya Palestina.
Hatua hii ni katika mwendelezo wa pande hizo mbili kubadilishana mateka na wafungwa chini ya makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Chini ya makubaliano hayo ya kusitishwa kwa mapigano, bidhaa muhimu kama vile, mafuta, chakula na misaada ya matibabu imeanza kuwasilishwa katika Ukanda wa Gaza.