Kwa nini utawala wa Kizayuni hautekelezi makubaliano ya kuondoka Lebanon?
Utawala wa Kizayuni baada ya kukabiliwa na upinzani mkubwa kutokana na kukataa kuondoa askari wake kusini mwa Lebanon katika muda uliopangwa, sasa umeanza kutoa tuhuma za uongo dhidi ya Iran.
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amezitaja tuhuma za Israel kuhusu kupelekwa nchini Lebanon mifumo ya hali ya juu ya silaha za Iran kuwa hazina msingi wowote na kuwa, utawala wa Israel unatoa tuhuma hizo zisizo na msingi ili kuhalalisha uvamizi wake haramu nchini humo.
Katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Amir Saeed Irawani ameeleza kuwa madai hayo si chochote ila ni kisingizio cha utawala wa Kizayuni cha kuhalalisha ukiukaji unaoufanya mara kwa mara wa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la mwaka 2006 na kutozingatia kwake maagizo ya usitishaji vita huko Lebanon. Amesema: "Kuhusishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na shughuli za uharibifu na uvunjifu wa amani katika eneo ni jambo lisilo na msingi na ni jaribio la makusudi na lililopangwa la kupotosha ukweli na kuwaondolea lawama watuhumiwa wakuu wa mauaji ya kimbari na jinai za kivita zinazofanywa na jeshi la Utawala wa Israel dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza."
Kwa mujibu wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa tarehe 27 Novemba 2024, Israel inalazimika kuondoka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu huko Lebanon ndani ya siku 60, yaani hadi leo Jumapili, Januari 26, lakini baraza la mawaziri la Netanyahu limeamua kuendelea kukalia ardhi ya nchi hiyo hata baada ya kumalizika kipindi hicho.
Kanali ya 11 ya utawala wa Kizayuni ilitangaza kuwa, mwishoni mwa kikao chake, baraza la mawaziri la utawala huo liliamua kurefusha muda wa usitishaji vita kwa mwezi mmoja na kuendelea kuwepo vikosi vya jeshi lake huko kusini mwa Lebanon.
Chanzo cha habari cha Israel pia kiliiambia CNN kwamba Baraza la Mawaziri la Israel limeifahamisha Washington kwamba vikosi vyake vitasalia kusini mwa Lebanon kwa angalau mwezi mwingine mmoja baada ya kumalizika muhula wa usitishaji mapigano.
Hata hivyo, tarehe ya mwisho iliyoombwa na baraza la mawaziri lenye itikadi kali la Netanyahu la kuondoka Lebanon limekabiliwa na upinzani mkali. Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema: "Tunaendelea kudai utekelezaji kamili wa Azimio nambari 1701 kama njia jumuishi kuelekea amani ya muda mrefu, usalama na utulivu katika pande zote mbili za Mstari wa Blue."
Rais Joseph Aoun wa Lebanon pia ameonya kuhusu matokeo ya kutofuata Tel Aviv maagizo ya makubaliano hayo na kuutaka utawala mpya wa Trump kutumia ushawishi wake kwa Netanyahu na kumlazimisha azingatie masharti ya makubaliano hayo.
Maurice Salim, Waziri wa Ulinzi wa Lebanon pia amesema: "Msimamo wa Lebanon juu ya kuondoka kwa majeshi ya Israel ni thabiti hadi mwisho wa muda uliowekwa (Januari 26)." Ameonya kuwa kukataa Israel kuondoka katika maeneo inayoyakalia kunatishia usalama wa Lebanon na eneo zima la Asia Magharibi.
Kuhusiana na hilo, Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon, katika kikao na Jenerali Jasper Jeffers, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufuatiliaji wa Usitishaji Vita, amesisitiza haja ya Israel kuzingatia azimio nambari 1701 na kuacha kulikiuka.
Hizbullah imechapisha taarifa ikizitaka nchi zinazounga mkono makubaliano hayo na jamii ya kimataifa kuiwekea mashinikizo Tel Aviv ili itekeleze ahadi zake kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano na kuondoka Lebanon baada ya kumalizika muda wa siku 60.
Jeshi la Israel limekataa kuondoka katika maeneo linayoyakalia kwa mabavu ya Lebanon, katika hali ambayo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita limefanya takriban mashambulizi 630 ya ndege zisizo na rubani, milipuko na uchomaji moto wa nyumba na majengo na kufanya operesheni za kusafisha na ufyatuaji risasi, jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano na Lebanon.
Ripoti za nyanjani pia zinaonyesha kuwa wanajeshi wa Israeli wanaendeleza operesheni zao katika maeneo ya makazi kusini mwa Lebanon. Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Lebanon, vikosi vya Israel viliingia katika makazi ya Bani Hayyan siku ya Ijumaa na kuharibu na kuchoma moto majengo ya makazi na ofisi katika eneo hilo. Pia, kulitokea mlipuko mkubwa katika mji wa "Rab Salasin" ambao ulisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu.
Kwa kuzingatia suala hilo, ni wazi kwamba muda ulioombwa na baraza la mawaziri la Netanyahu hautakuwa wa mwezi mmoja tu na kwamba utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine utakiuka wajibu wake na kuendelea kukalia kwa mabavu maeneo ya kusini mwa Lebanon.