Umoja wa Mataifa: Shirika la UNRWA halina mbadala
Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika barua yake kwa Israel kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA haliwezi kuwa na mbadala na kwamba na litaendelea kufanya kazi zake huko Palestina.
Stephen Dujarric ameeleza kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemtumia barua balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Danny Denon, ambapo amefafanua msimamo wetu kwa kuzingatia sheria za kimataifa, shughuli muhimu ya UNRWA haiwezi kubadilishwa katika nyanja nyingi.
Dujarric aliongeza: Shughuli za UNRWA zitaongezeka hata baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza, na hatutaki kuhatarisha shughuli zetu za kibinadamu huko. UNRWA ina misheni na jukumu kutoka Umoja wa Mataifa na lazima itimize jukumu hili.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni wa Israel umesema kuwa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lina hadi mwisho wa mwezi huu wa Januari kuondoka katika mji mtukufu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu.
Utawala haramu wa Israel umehalalisha hatua yake hiyo kwa kuibua madai yasiyo na msingi kwamba, UNRWA, ambayo imekuwa ikiwaunga mkono Wapalestina tangu 1949, eti inaajiri wafanyakazi wanaoshiriki katika shughuli za kigaidi.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina limekuwa likisisitiza kuwa, hakuna taasisi yoyote inayoweza kujaza nafasi ya shirika hilo katika kuwahudumia na kuwafikishia misaada wakimbizi wa Kipalestina.