Israel inaendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano Lebanon
(last modified Sun, 16 Feb 2025 14:00:44 GMT )
Feb 16, 2025 14:00 UTC
  • Israel inaendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano Lebanon

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeshambulia kusini mwa Lebanon na kudai kuwa umemuua mmoja wa makamanda wa kikosi cha anga cha Hizbullah.

Licha ya kutangazwa makubaliano ya usitishaji vita kati ya Lebanon na utawala wa Kizayuni, lakini utawala huo ghasibu unaendelea kuingilia masuala ya ndani ya Lebanon, kukiuka mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo na kuyashambulia kwa mabomu maeneo mbalimbali nchini humo.

Televisheni ya al Mayadeen jana usiku ilitanagza kuwa watu wawili wameuliwa shahidi na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya gari moja katika kitongoji cha Jarhouh huko Lebanon. 

Yisrael Katz Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel amedai kuwa wamemuua kamanda mmoja wa vikosi vya anga vya harakati ya Hizbullah katika shambulio hilo. 

Wakati huo huo, Ibrahim Mousavi mwakilishi katika Bunge la Lebanon amejibu vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Isarel kuhusu kushambulia ndege ya abiria ya Iran iliyobeba raia wa Lebanon na kusema: Chokochoko za utawala wa Kizayuni dhidi ya mamlaka ya kujitawala ya Lebanon na himaya ya baadhi ya nchi za Magharibi hasa Marekani kwa utawala huo vinazidi kuutia kiburi utawala huo cha kuendelea kufanya uhalifu. 

"Kila mtu nchini Lebanon lazima alaani kwa sauti kubwa na kuzishinikiza taasisi husika za kimataifa ili ziuchukulie hatua utawala wa Kizayuni," amesema mbunge huyo wa Lebanon.