Ripoti: Marekani na Ufaransa zinataka askari mamluki wapelekwe kusini mwa Lebanon
(last modified Wed, 19 Feb 2025 06:54:18 GMT )
Feb 19, 2025 06:54 UTC
  • Ripoti: Marekani na Ufaransa zinataka askari mamluki wapelekwe kusini mwa Lebanon

Marekani na Ufaransa zimeripotiwa kuwa zimependekeza mamluki wanaoitwa wakandarasi binafsi wapelekwe kusini mwa Lebanon katika jitihada za kuushawishi utawala wa Kizayuni wa Israel uondoe kikamilifu majeshi yake nchini humo.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya habari ya Middle East Eye (MEE) ambayo imesema: "Ufaransa na Marekani zinajaribu kuishawishi Israel iondoke kikamilifu kusini mwa Lebanon kwa kupendekeza kutumwa kikosi cha kulinda amani au hata makampuni ya usalama ya binafsi katika maeneo ya kimkakati".
 
Duru ya kidiplomasia ya Marekani imesema, Israel inataka kubaki kusini mwa Lebanon kwa uchache hadi Februari 28 ili "kusimamia kurejea kwa salama" walowezi wa Kizayuni katika makazi ya kaskazini, ambao walilazimika kukimbia kutokana na operesheni za Muqawama wa Hizbullah.
 
Kipindi cha uhamiaji huo kinatarajiwa kumalizika mwanzoni mwa Machi.
 
Duru moja ya kidiplomasia imeitaarifu MEE kuwa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwasiliana na Rais wa Lebanon Joseph Aoun na kuwafahamisha Waisraeli" kwamba Lebanon inapinga kikamilifu jeshi la Kizayuni kuendelea kuwepo kusini mwa nchi hiyo".
 
Duru hiyo imeongezea kueleza kwamba, Ufaransa ilipendekeza kupeleka wanajeshi wake au walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo.
 
Hata hivyo kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon Youssef Rajji utawala wa Kizayuni wa Israel uliukataa mpango huo uliopendekezwa na Ufaransa.
 
Duru nyingine ya kidiplomasia ya Marekani imesema Washington ilipedekeza kupeleka vikosi vya kimataifa au wakandarasi binafsi, wazo ambalo inadaiwa kuwa limepingwa na Lebanon.
 
Mamluki wa Marekani kwa sasa wanahudumu katika Ukanda wa Ghaza, ambako kuna usitishaji tete wa mapigano baada ya mwaka mmoja wa mauaji ya kimbari yaliyofanywa na jeshi la utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
 
Wakati huo huo, katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jana Jumanne, viongozi wa Lebanon walitilia mkazo tena msimamo mmoja wa kitaifa ilionao nchi hiyo kuhusiana na mwenendo wa utawala wa Kizayuni.
 
Viongozi wa Lebanon wamesisitizia haja ya ulazima wa Israel kuondoka kikamilifu katika ardhi ya nchi hiyo kwa mujibu wa maazimio ya kimataifa, hususan azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.../