Misri yakataa pendekezo la Wazayuni la kuitawala Gaza kwa miaka 8
Cairo imekataa pendekezo la maafisa wa utawala za Kizayuni wa Isarel wanaotaka serikali ya Misri isimamia mamlaka ya Ukanda wa Gaza kwa miaka 8 hadi 15.
Ripoti za vyombo vya habari vilivyo karibu na Wazayuni zinasema kuwa mustakabali wa utawala wa Gaza ndilo suala muhimu zaidi ambalo Israel inalifuatilia kwa sasa.
Ingawa Tel Aviv imelipa kipaumbele suala la kufuta kizazi cha Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, lakini inaonekana kuwa, miongoni mwa machaguo mengine ya utawala huo ghasibu kuhusu eneo hilo ni kutafuta nchi na makundi mengine yatakayosimamia mamlaka ya eneo hilo badala ya Hamas.
Ripoti zinasema Cairo imekataa pendekezo la sasa la Israel baada ya Yair Lapid, kiongozi wa wapinzani wa Netanyahu, kupendekeza kuwa Misri itawale Gaza kwa miaka 8.
Vyanzo vya vya Misri, ambavyo havikutaka kutajwa majina, vimeiambia Al Arabiya kwamba: Cairo inapinga mpango wowote wa kuitawala Gaza. "Hatuna nia ya kutawala ukanda huu, na ni Wapalestina peke yao ambao hatimaye wanapaswa kuamua juu ya suala hili", kimesema chanzo hicho.
Lapid alipendekeza kuwa Gaza itawaliwe na Misri kwa miaka 8 wakati wa mchakato wa ujenzi mpya na kwamba usimamizi huo unaweza kurefushwa hadi miaka 15.