Hamas yalaani ya mashambulizi ya Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani vikali mashambulizi ya anga ya Marekani na Uingereza dhidi ya maeneo ya makazi ya watu huko Sana'a, mji mkuu wa Yemen.
Hamas imetoa taarifa na kulaani vikali mashambulizi ya kihalifu ya anga ya Marekani na Uingereza dhidi ya maeneo ya raia katika mji mkuu wa Yemen. Hamas imesema hujuma hizo za Marekani na Uingereza zimekiuka wazi sheria za kimataifa na pia mamlaka ya kujitawala ya nchi ndugu ya Yemen.
Hamas imetangaza uungaji mkono wake kamili kwa wananchi na serikali ya Yemen na kupongeza msaada na hatua za Yemen za kuwahami wananchi wa Palestina wa Ukanda wa Gaza wakati wa vita na mauaji ya kimbari ya Israel.
Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen nayo ilikuwa imetoa taarifa baada ya jinai hizo za aga za Marekani na Uingereza na kuyataja mashambulizi ya nchi hizo mbili dhidi ya makazi ya raia katika mji wa Sana'a kuwa ni kitendo cha uhasama na ni jinai.
Taarifa ya Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah imesema: Kulenga raia na vitongoji vya makazi ya raia ni jinai kamili ya kivita na ishara nyingine ya ugaidi wa Marekani dhidi ya mataifa na nchi pinzani duniani.
Jumamosi na mapema leo Marekani na Uingereza zimefanya mashambulizi makubwa ya kijeshi katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a na mikoa ya Sa'ada, Dhamar, Hajjah na al-Bayda.
Kwa akali watu 31, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa katika mashambulizi hayo ya anga na majini yaliyoagizwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Wapiganaji wa Ansarullah wamejibu mapigo kwa kushambulia meli kubwa ya kubeba ndege za kivita ya Marekani, Harry S. Truman kwa mara ya pili katika muda wa saa 24.
Msemaji wa jeshi la Yemen, Yahya Saree amesisitiza azma ya harakati hiyo la kuzuia meli zote zinazoelekea au kutoka Israel kusafiri katika eneo la operesheni hadi utawala huo utakapoondoa mzingiro kwa watu wa Ukanda wa Gaza.