Israel yapigwa na makombora kutoka Yemen, ving'ora vyahanikiza
Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimevurumisha makombora kuelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, na kuwatia kiwewe na hofu Wazayuni; huku safari za ndege zikisimamishwa Tel Aviv.
Shambulizi hilo la wanajeshi wa Yemen limepelekea kusikika mara kadhaa ving'ora vya tahadhari mjini Tel Aviv na viunga vyake, na kuwalazimisha maelfu ya walowezi wa Kizayuni kukimbilia kwenye mahandaki.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, ving'ora vimesikika pia katika majiji na miji zaidi ya 20 inayokaliwa kwa mabavu, ikiwa ni pamoja na Al-Quds, na kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.
Televisheni ya Almasirah pia imetangaza kuwa, sauti za ving'ora zimerindima huko Jaffa, uwanja wa ndege wa kijeshi wa Palmachim kusini mwa Jaffa inayokaliwa kwa mabavu, na maeneo mengine ya Palestina yaliyoghusubiwa.
Jeshi la Israel linadai kwamba makombora yalilorushwa kutoka Yemen yametunguliwa na jeshi lake la anga "kabla ya kutua ardhini."
Shambulio hilo lilizusha tahadhari za mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel. kadhalika safiri za ndege zimesitishwa katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion kufuatia shambulio hilo la makombora kutoka Yemen.
Haya yanajiri baada ya Vikosi vya Ulinzi vya Yemen (YAF) kutangaza kuwa, Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion wa Israel sasa hauko salama kwa usafiri wa anga, na utaendelea kuwa hivyo hadi uchokozi wa utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Gaza utakapokomeshwa na vizuizi vya misaada lilivyoekewa eneo hilo la Palestina vitakapoondolewa.