Hamas: Mauaji ya Wapalestina akiwemo Mbunge yataimarisha Muqawama
Jeshi la Israel limefanya mashambulizi mapya ya kutisha ya anga katika Ukanda wa Gaza na kuua shahidi watu wasiopungua 40, akiwemo Salah al-Bardawil, Mbunge wa Palestina na Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumapili, Hamas imesema kuwa Bardawil alilengwa katika operesheni ya "mauaji ya kihaini ya Wazayuni", alipokuwa akiswali usiku wa kuamkia tarehe 23 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Bardawil aliuawa shahidi pamoja na mke wake katika shambulio hilo la anga la Israel lililolenga hema lake katika eneo la al-Mawasi, magharibi mwa mji wa Khan Yunis, kusini wa Gaza
Kundi hilo la Muqawama pia limemsifu Bardawil na kumtaja kama 'nembo ya kisiasa, vyombo vya habari, na kazi ya kitaifa,' na kubainisha kwamba "hakuwahi kushindwa kutekeleza majukumu yake au jihadi (jitihada kwa ajili ya Mungu)" kwa lengo la kukuza kadhia ya Palestina.
Hamas imesisitiza kuwa, utawala huo wa kihalifu hautadhoofisha azimio na uthabiti wa Wapalestina kwani "kwa kila anayeuawa shahidi, moto wa Muqawama unazidi kuwa na nguvu hadi pale ukaliaji wa mabavu (wa ardhi ya Palestina) utakapomalizika."

Wamorocco waandamana Rabat kuonyesha uungaji mkono wao kwa Palestina na kupinga mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza
Wakati huo huo duru za hospitali zimetangaza kuwa, Wapalestina wasiopungua 40 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita.
Maandamano yanaendelea kushuhudiwa katika miji mbali mbali duniani kote, ikiwemo miji ya Rabat na Marrakesh nchini Morocco, kulaani mauaji ya Wapalestina karibu 600, wakiwemo watoto zaidi 200, mbali na wengine wapatao 1,000 kujeruhiwa huko Gaza tangu jeshi la Kizayuni lilipovunja makubaliano ya usitishaji mapigano Jumanne na kuanzisha hujuma mpya.