Ripoti: Israel imeua wanahabari wa Kipalestina 212 tangu Oktoba, 2023
(last modified Sat, 26 Apr 2025 02:38:37 GMT )
Apr 26, 2025 02:38 UTC
  • Ripoti: Israel imeua wanahabari wa Kipalestina 212 tangu Oktoba, 2023

Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza imesema, kutokana na mauaji ya mwanahabari Saeed Amin Abu Hassanein, idadi ya waandishi wa habari wa Palestina waliouawa shahidi na Israel imeongezeka hadi 212, tangu vita vya mauaji ya kimbari vilipoanza katika eneo hilo lililozingirwa mnamo Oktoba mwaka 2023.

Katika taarifa, ofisi hiyo imesema tangazo hilo linakuja baada ya Israel kushambulia hema la waandishi wa habari katika Hospitali ya Nasser, na kusababisha kuuawa mwandishi wa habari Hilmi al-Faqawi na Hassanein, ambaye amefariki dunia kutokana na majeraha.

"Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza inalaani vikali kulengwa, kushambuliwa na kuuawa kigaidi kwa waandishi wa habari wa Kipalestina na utawala ghasibu wa Israel," imesema taarifa hiyo.

"Tunatoa wito kwa Shirikisho la Kimataifa la Waandishi wa Habari, Jumuiya ya Waandishi wa Habari wa Kiarabu, na vyombo vyote vya uandishi wa habari katika nchi zote duniani kulaani uhalifu huu wa kimfumo dhidi ya wanahabari wa Kipalestina na wataalamu wa vyombo vya habari katika Ukanda wa Gaza," imeongeza taarifa hiyo.

Februari mwaka huu, Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari nchini Marekani sambamba na kutangaza kuwa, idadi kubwa ya waandishi wa habari waliuawa duniani kote mwaka jana, ilieleza kwamba, utawala wa Israel ulihusika na mauaji ya takriban asilimia 70 ya waandishi hao.

Waandishi wa habari ni miongoni mwa wahanga wakuu wa mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza. Jinai iliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita vyake dhidi ya Gaza haina mfano wake katika vita vya miongo ya hivi karibuni.

Wakati wa uvamizi wa Marekani dhidi ya Vietnam, ambao ulidumu karibu miaka 20, waandishi wa habari 63 waliuawa, huku waandishi wa habari 17 wakiuawa katika Vita vya Peninsula ya Korea vilivyodumu kwa muda wa miaka 3.