Ansarullah: Israel haielewi lugha nyingine isipokuwa ya makombora
Kwa mara nyingine tena Harakati ya Muqawama ya Ansarullah imevurumisha kombora la balestiki kutoka Yemen na kupelekea sauti za ving'ora kuhanikiza katika maeneo mengi katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ikiwemo miji mikubwa, mbali na kuibua miripuko kadhaa.
Kombora hilo lilirushwa kuelekea katika maeneo hayo mapema leo Jumapili, huku jeshi la Israel likiripoti kuwa limeelewa na kupata wakati mgumu kujaribu kulitungua.
Sauti za ving'ora vya tahadhari zilihanikiza katika miji ya Tel Aviv, mji mtakatifu wa al-Quds unaokaliwa kwa mabavu, na Netanya miongoni mwa maeneo mengine.
Katika taarifa yake kufuatia shambulio hilo, Nasr al-Din Amer, afisa wa ngazi ya juu katika Harakati ya Ansarullah ameashiria hatua ya utawala haramu wa Israel kutotilia maanani miito ya Waarabu ya kutaka amani na kusisitiza kuwa, miripuko inayosikika katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu ndiyo lugha pekee ambayo utawala huo unaielewa.
"Wazayuni hawakusikiliza sauti ya mkutano wa kilele wa Waarabu na hawakuizingatia," amesema Amer na kuongeza kuwa, "Sasa, hii ndiyo sauti inayosikika - milipuko inayosikika ndani kabisa ya shirika la Kizayuni."
Afisa huyo mwandamizi wa Ansarullah ameongeza kuwa, "Hii ndiyo lugha ambayo utawala huo (wa Kizayuni) unaelewa, na (lugha hii) inasimamiwa na kuendeshwa na watu wa Allah huko Yemen."
Ansarullah imeapa kwamba wanajeshi wa Yemen wataendelea kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa hujuma za Israel dhidi ya ardhi za Palestina na Yemen kwenyewe.