Hamas: Nchi za Kiarabu zichukue hatua kumaliza mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, imewataka viongozi wa nchi Kiarabu kuchukua hatua za haraka na za kiutendaji ili kumaliza mashambulizi yanayoendelea ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuondoa vizuizi vya kibinadamu vinavyosababisha maafa katika eneo hilo lililozingirwa.
Hamas ilitoa wito huo katika taarifa siku ya Jumamosi, wakati Mkutano wa 34 wa Kilele wa Jumuiya ya Kiarabu ambao umefanyika Jumamosi katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ambapo mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Gaza yalikuwa mada kuu.
Hamas ilisema Ukanda wa Gaza unakabiliwa na mojawapo ya mashambulizi mabaya zaidi katika historia na yenye umwagaji damu mkubwa. Utawala vamizi wa Israel unaendelea kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya raia, ukilenga maeneo ya makazi na vituo vya hifadhi, na kusababisha kufa shahidi na kujeruhiwa kwa mamia ya watu, huku ukiwa chini ya mzingiro mkali na kusitishwa kabisa kwa misaada ya kibinadamu.
Harakati hiyo imeendelea kusema kuwa hasa Kaskazini mwa Gaza inashuhudia "kampeni ya mauaji ya kimfumo," na mashambulizi makali ya anga na ya mizinga yanayolazimisha mamia ya familia kuhama kwa lazima kutoka makazi yao, wakikimbia kifo na mashambulizi.
Israel ilianzisha kampeni ya mauaji ya kimbari huko Gaza tarehe 7 Oktoba 2023. Hadi sasa, imeua zaidi ya Wapalestina 53,000, wengi wakiwa ni wanawake na Watoto.
Mnamo Januari, utawala wa Israel ulilazimika kukubali makubaliano ya kusitisha mapigano na Hamas, kutokana na kushindwa kufanikisha malengo yake Gaza, ikiwa ni pamoja na "kuangamiza" harakati ya Hamas au kuwaachilia mateka.
Mnamo Machi 18, utawala huo ulianzisha tena mashambulizi dhidi ya Gaza, ukikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na kubadilishana wafungwa yaliyoendelea kwa karibu miezi miwili.