Hamas: Tutaendeleza mapambano hadi tone la mwisho la damu
Msemaji wa Brigedi za al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesisitiza kwamba operesheni za wanamuqawama dhidi ya uvamizi wa Israel zitaendelea "hadi pale utawala wa Kizayuni utakaposhindwa."
Abu Ubaida amesema hayo katika taarifa ya jana Ijumaa na kueleza kuwa, "Wapiganaji wetu, warithi wa Mitume, wanaendelea kuyarushia Mawe ya (Nabii) Daud (AS) Magari ya Gideon, na kuangusha ubeberu wa uvamizi huo hadi utakaposhindwa."
Amepongeza uthabiti wa wapiganaji wa Muqawama akisema kwamba, kupitia ushujaa wao, "wanasajili ushindi wa waaminifu na wanaokandamizwa juu ya wenye kiburi na madhalimu."
Akizungumzia shambulizi la kuvizia la Ijumaa asubuhi katika mji wa kusini wa Gaza wa Khan Yunis, ambalo lilisababisha vifo vya wanajeshi watano wa Israel na wengine kujeruhiwa, Abu Ubaida amesema, "hasara iliyoletwa kwenye uvamizi wa leo (jana) huko Khan Yunis na Jabalia ni mwendelezo wa mfululizo wa operesheni sahihi - mfano wa kile kinachongojea majeshi vamizi popote yanapokanyaga."
Makundi ya Muqawama ya Wapalestina yalifanya msururu wa operesheni zenye mafanikio katika eneo la Khan Yunis siku ya Ijumaa, zikilenga maeneo muhimu ya kijeshi ya Israel, wakati ambapo utawala wa Kizayuni unapoendeleza mashambulizi ya kinyama katika Ukanda wa Gaza.
Wapiganaji wa Kikosi cha Al-Quds wakishirikiana na Kikosi cha Hamas cha Al-Qassam, walishambulia makao makuu ya utawala huo ghasibu wa Israel karibu na Ukumbi wa Canada kusini mashariki mwa Khan Yunis kwa wimbi la maroketi.
Katika operesheni tofauti, wapiganaji wa Muqawama waliharibu gari la kijeshi la Israel kwa kutumia mada za miripuko za IED katika eneo la Kafr Qarara kaskazini mwa Khan Yunis.