Netanyahu aapa hakutakuwa na Dola la Palestina, asisitiza ardhi yote ni milki ya wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130716-netanyahu_aapa_hakutakuwa_na_dola_la_palestina_asisitiza_ardhi_yote_ni_milki_ya_wazayuni
Waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwa, hakutakuwa na dola la Palestina, na kusisitiza kwamba ardhi zote za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu ni milki ya wazayuni.
(last modified 2025-09-12T06:58:37+00:00 )
Sep 12, 2025 06:58 UTC
  • Netanyahu aapa hakutakuwa na Dola la Palestina, asisitiza ardhi yote ni milki ya wazayuni

Waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ameapa kuwa, hakutakuwa na dola la Palestina, na kusisitiza kwamba ardhi zote za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu ni milki ya wazayuni.

Netanyahu alitoa kauli hiyo Alkhamisi alipozungumza katika hafla ya utiaji saini mradi mkubwa wa ujenzi haramu wa vitongoji iliyofanyika katika eneo la Maale Adumim karibu na Baitul Muqaddas Mashariki inayokaliwa kwa mabavu. 

Waziri mkuu wa utawala wa kizayuni amesema: "tutatimiza ahadi yetu kwamba hakutakuwa na dola la Palestina, mahala hapa ni petu".

Katika tukio hilo lililoonyeshwa mubashara na ofisi yake, Netanyahu ameendelea kubainisha: "tutalinda urithi wetu, ardhi yetu na usalama wetu... tutaongeza maradufu idadi ya watu wa jiji hili." 

Utawala wa kizayuni umekuwa na ndoto ya kujenga vitongoji kwenye eneo la kilomita za mraba zipatazo 12 linalojulikana kama E1, lakini mpango huo ulikuwa umekwama kwa miaka mingi kutokana na upinzani wa kimataifa.

Eneo hilo liko kati ya Baitul Muqaddas Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na vitongoji haramu vya walowezi wa kizayuni vya eneo la Maale Adumim, karibu na njia zinazounganisha kaskazini na kusini mwa ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Jamii ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa, inautambua ujenzi wa vitongoji unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel kuwa ni haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Umoja wa Mataifa umeshaonya mara kadhaa kwamba kuendelea kupanuliwa ujenzi wa vitongoji hivyo kunahatarisha uwezekano wa suluhisho la mataifa mawili, mfumo unaoonekana kuwa muhimu katika kutatua mzozo wa miongo kadhaa kati ya Palestina na utawala wa kizayuni unaosisitizia haki ya Wapalestina kuwa na nchi yao huru kulingana na mipaka ya mwaka 1967, na ambayo mji mkuu wake utakuwa ni Baitul Muqaddas Mashariki.../