Jumatatu tarehe Mosi Juni 2026
Leo ni Jumatatu 15 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1447 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Juni 2026.
Siku kama ya leo miaka 1233 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Ali Naqi (AS) mashuhuri kwa lakabu ya al-Hadi, mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW, katika mji mtakatifu wa Madina.
Baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Jawad AS, Imam Hadi alichukua jukumu zito la Uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu. Zama za Uimamu wake zilisadifiana na kipindi cha utawala wa ukoo wa Bani Abbas, na Mutawakkil ndiye aliyekuwa ameshika hatamu za uongozi wakati huo.
Baada ya mtawala huyo kuhisi kuwa Imam Hadi (as) na wafuasi wake walikuwa hatari kwa utawala wake, aliamrisha Imam atolewe Madina na kuhamishiwa Samarra, Iraq ili amuweke chini ya uangalizi. Licha ya hayo yote, lakini Imam Naqi aliendelea kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 366 iliyopita Mary Barrette Dyer, ambaye alikuwa mhubiri wa Quakerism huko Marekani, alinyongwa na mahakama ya Massachusetts kwa sababu za kidini.
Wakati huo, sheria ya Massachusetts ilikataza Maquakers kuingia eneo hilo. Wafuasi wa kundi hilo wanaojulikana kama Quakers ni watu waliokuwa katika kundi la kihistoria la Kikristo la Kiprotestanti linalojulikana kama Jumuiya ya Kidini ya Marafiki.
Quakerism iliibuka katika karne ya 16 na 17 kama jibu kwa hitilafu na vita vya kidini vilivyotokea huko Ulaya na vilevile uhasama na mizozo baina ya madhehebu ya Kikristo nchini Uingereza. George Fox alikuwa mmoja wa wahubiri mashuhuri wa kundi hilo. Kundi hili lilienea polepole katika ulimwengu wa Kikristo.
Quakers waliamini katika kurahisisha shughuli za kidini na kwamba kanisa halipaswi kuwa na mchungaji maalumu na anayelipwa mshahara na kuwa kiunganishi na wasita kati ya Mungu na Mtume wake kwa upande mmoja, na watu wa kawaida kwa upande mwingine. Waliamini kuwa mahubiri na mafundisho ya Kikristo yanapaswa kufanywa kwa hiari na kila mtu mwenye ujuzi. ***
Siku kama ya leo tarehe Mosi Juni miaka 74 iliyopita, aliaga dunia John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Alihitimu falsafa katika Chuo Kikuu cha Vermont kabla ya kuwa na umri wa miaka ishirini, na baada ya kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya falsafa, alifundisha katika Chuo Kikuu cha Columbia. Dewey alibobea mno katika taaluma ya elimu na malezi. Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na elimu na malezi. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture." John Dewey alifariki dunia mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93. ***
Miaka 100 iliyopita muwafaka na siku kama ya leo, moja kati ya zilzala kubwa zilizouwa watu wengi duniani, iliikumba Tokyo mji mkuu wa Japan.
Zilzala hiyo ilitokea nyakati mbili tofauti kwa kupishana muda mfupi. Mtetemeko huo wa ardhi uliharibu nusu ya mji wa Tokyo na kuuwa watu zaidi ya laki moja na elfu hamsini. ***
Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, Ustadh Seyyed Hossein Mirkhani, mmoja wa waanzilishi wa Jumuiya ya Waandishi wa Hati Nzuri Iran na mwalimu mahiri wa wa maandishi ya Nastaliq, aliaga dunia baada ya juhudi za maisha yake yote katika fani ya calligraphy. Mwalimu Mirkhani alizaliwa mwaka wa 1286 Hijria Shamsia na akaanza kufanya mazoezi ya kuandika maandishi akiwa mtoto, na kufikia umri wa miaka kumi na moja alikuwa na mwandiko mzuri. Hossein Mirkhani alitumia miaka 30 ya maisha yake kuwaelimisha na kuwafunza wanafunzi wa kaligrafia. Mbali na ubunifu wake wa kisanii, Profesa Mirkhani pia alikuwa na maadili mema. Aliandika Kurani Tukufu kwa hati ya Nastaliq mara tatu wakati wa uhai wake.
Katika siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Chama cha Jamhuri ya Kiislamu, kikiwa chama kikubwa na kilichojumuisha watu wengi zaidi nchini Iran baada ya mapinduzi, kilivunjwa kwa pendekezo la wanachama wake. Chama cha Jamhuri ya Kiislamu kilianzishwa wiki moja baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Iran na Seyyed Mohammad Hosseini Beheshti, Seyyed Ali Khamenei (kiongozi wa sasa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran), Seyyed Abdolkarim Mousavi Ardebili, Akbar Hashemi Rafsanjani, na Dk. Muhammad Javad Bahonar.