Jihad Islami Palestina kuendeleza mapambano ya kukomboa Quds
Afisa wa ngazi za juu wa harakati ya kupigania ukombozi Palestina ya Jihad Islami amesisitiza udharura wa kuendelezwa mapambano na mwamko (Intifadha) dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ili kukomboa ardhi zote za Palestina hasa Quds Tukufu (Jerusalem).
Khader Adnan mwanachama wa ngazi za juu katika Jihad Islami amesema Intifadha itaendelea kwa mbinu mbalimbali huko Palestina maadamu ardhi za Palestina zinakaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Ameongeza kuwa Wapalestina wameazimia kuendeleza Intifadha kwani licha ya kuwepo hatua kali za usalama zilizochukuliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel, mapambano ya Wapalestina yangali yanaendelea.
Afisa huyo wa Jihad Islami amesema, kususia kula mateka Wapalestina wanaoshikiliwa katika korokoro za Israel ni mojawapo ya mbinu za mapambano na Intifadha.

Maeneo mbalimbali ya Palestina yamekuwa yakishuhudia mapambano makali tokea Oktoba mwaka 2015 ambapo Wapalestina wanalalamikia ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel na njama za kuuyahudisha mji wa Quds na kuharibu Msikiti wa Al Aqsa ambao ni qibla cha kwanza cha Waislamu.
Kufuatia ukatili wa wanajeshi wa Israel, tokea wakati huo hadi sasa Wapalestina zaidi ya 230 wameuawa shahidi.