Oct 12, 2016 07:53 UTC
  • Magaidi washambulia msikiti Kabul na kuua makumi usiku wa Tasua

Kundi moja la kigaidi na kitakfiri nchini Afghanistan limefanya shambulizi la pili dhidi ya Waislamu wa madhebu ya Shia waliokuwa wamekusanyika msikitini wakifanya maombelezo ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS.

Habari zinasema kuwa, magaidi hao wameshambulia Msikiti wa Char Yar ulioko katika eneo la Karte Char, viungani mwa mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na kuua idadi kubwa ya watu huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Sediq Sediqi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan amesema shambulizi hilo la jana usiku limejiri masaa machache baada ya magaidi wanne wa kitakfiri kuwashambulia kwa risasi waombolezaji waliokuwa wamekusanyika katika Haram ya Karte Sakhi mjini Kabul, wakati wa maadhimisho ya Tasua hapo jana na kuua 14 miongoni mwao huku wengine 36 wakijeruhiwa.

Athari za hujuma za kinyama Kabul

Hakuna kundi lolote la kigaidi likiwemo la Taliban lililotangaza kuhusika na ukatili huo wa Kabul, dhidi ya waombolezaji wanaokumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW.

Itakumbukwa kuwa, mwezi Julai mwaka huu, Waislamu wasiopungua 80 waliuawa na wengine zaidi ya 231 kujeruhiwa katika shambulizi la bomu lililofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh dhidi ya maandamano ya amani ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Tags