Makumi wauawa na kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi Iraq
Watu zaidi ya 30 wameuawa na kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi lililoulenga mkusanyiko wa waombolezaji waliokuwa wakiandamana katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad.
Habari zinasema kuwa, gaidi wa kujitolea muhanga alijiripua alipofika kwenye mkusanyiko huo wa watu, kaskazini mwa Baghdad na kuua 6 miongoni mwao huku wengine zaidi ya 21 wakijeruhiwa. Duru zingine za habari zimearifu kuwa, waliouawa katika hujuma hiyo ya leo ya Baghdad ni watu zaidi ya 20.
Shambulizi la leo limejiri siku moja baada ya hujuma nyingine ya kinyama kusababisha vifo vya watu zaidi ya 50 katika wilaya ya al-Sha’ab, viungani mwa Baghdad. Wimbi hili la mashambulizi ya kigaidi linaonekana kuwa hujuma za kulipiza kisasi kutoka matakfiri wa Daesh/ISIS.
Mwezi uliopita, wanachama wasiopungua 100 wa kundi la kigaidi la Daesh waliuawa nchini Iraq kufuatia mashambulio ya anga yaliyofanywa na ndege za kijeshi za nchi hiyo katika mkoa wa al-Anbar, magharibi mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Katika siku za hivi karibuni wanajeshi wa Iraq wakishirikiana na jeshi la kujitolea na wananchi wamefanikiwa kuyakomboa maeneo mengi ya nchi hiyo yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.