UNICEF yatiwa wasiwasi na hali mbaya ya watoto nchini Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17680-unicef_yatiwa_wasiwasi_na_hali_mbaya_ya_watoto_nchini_yemen
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umesema una wasiwasi juu ya hali mbaya ya watoto wadogo katika nchi iliyokumbwa na vita na mgogoro ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 18, 2016 15:10 UTC
  • UNICEF yatiwa wasiwasi na hali mbaya ya watoto nchini Yemen

Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) umesema una wasiwasi juu ya hali mbaya ya watoto wadogo katika nchi iliyokumbwa na vita na mgogoro ya Yemen.

Msemeaji wa UNICEF nchini Yemen Muhammad al-As'adi ameelezea wasiwasi wa shirika hilo juu ya taathira za vita vinavyoendelea kwa watoto wa nchi hiyo na kueleza kwamba vita vya kutwishwa vilivyoanzishwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen vimesababisha watoto zaidi ya elfu moja kuuawa na wengine wapatao elfu mbili kujeruhiwa nchini Yemen.

Watoto wa Yemen katika maisha ya ukimbizi

Msemaji huyo wa UNICEF amebainisha kuwa raia milioni 21 wa Yemen wakiwemo watoto wapatao milioni 10 wanahitaji misaada ya kibinadamu na wengine wasiopungua milioni 19, nusu yao wakiwa ni watoto wadogo wanahitaji huduma na suhula za haraka za kiafya.

Al-As'adi ameongeza kuwa skuli zipatazo laki nane zimeharibiwa au kubomolewa kikamilifu katika mashambulio yaliyofanywa na Saudia na waitifaki wake na maelfu ya wanafunzi wamekosa masomo.

Kwa mujibu wa msemaji wa UNICEF asilimia 51 ya raia wa Yemen, yaani zaidi ya watu milioni 14 wanateseka na kutaabika kutokana na kurefuka muda wa vita na kuzidi kuwa mbaya hali ya uchumi wa nchi hiyo.

Miundombinu ya Yemen pia imeangamizwa na mashambulio ya Saudia 

Tangu mwezi Machi 2015 na kwa msaada wa baadhi ya nchi za Kiarabu na Marekani, utawala wa kifalme wa Aal Saud unaotawala nchini Saudi Arabia umeanzisha vita dhidi ya Yemen kwa lengo la kumrejesha madarakani kibaraka wake, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi Abdrabbuh Mansour Hadi.

Mashambulio hayo ya kinyama ya Saudia hadi sasa yameshaua zaidi ya Wayemeni elfu kumi, kujeruhi mamia ya maelfu ya wengine au kuwaacha bila ya makazi mbali na kuteketeza asilimia 80 ya taasisi za miundombinu na za utoaji huduma na tiba za nchi hiyo masikini ya Kiarabu.../