Zarif: Muqawama umesambaratisha njama za magaidi Lebanon
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema harakati za kimuqawama ndizo zimesambaratisha njama za maadui na magaidi nchini Lebanon.
Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake na Rais mpya wa Lebanon Michel Aoun mjini Beirut na kuongeza kuwa, maadui wa Iran na Lebanon ni wamoja: Utawala wa Kizayuni na magenge ya kitakfiri; lakini pamoja na hayo, Tehran na Beirut zimesimama bega kwa bega na kushirikiana kwa kila namna kuwakabili maadui hao.
Sanjari na kutoa mkono wa pongezi kwa Michel Aoun kwa kuchaguliwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya Kiarabu, Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekariri kuwa, Jamhuri ya Kiislamu daima imejitolea kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Lebanon katika nyuga mbali mbali.
Mbali na kukutana na Rais Michel Aoun, Zarif alikutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Lebanon, Gebran Bassil na kuzungumzia masuala ya kieneo na kimataifa.
Akihutubia waandishi wa habari akiwa pamoja na Bassil, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliutaka utawala wa kifalme wa Saudi Arabia kuacha sera zake za kiadui na uhasama; na kuchangia katika vita dhidi ya ugaidi wa makundi ya kitakfiri na yenye misimamo ya kufurutu ada na kubainisha kuwa, aidioliojia ya Uwahabi sio tishio tu kwa Iran, Lebanon na eneo la Mashariki ya Kati, bali kwa nchi zote duniani.