Nov 24, 2016 02:55 UTC
  • HRW yakosoa hali ya haki za binadamu katika nchi za Kiarabu

Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti na kulalamikia hali ya haki za binadamu katika nchi za Kiarabu likisema ni ya kutisha.

Shirika la habari la IRNA limelinukuu shirika hilo la kimataifa la haki za binadamu likilalamikia hali ya haki za binadamu katika nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi na kuzituhumu nchi hizo kuwa hazichungi hata viwango vya chini kabisa vya haki za binadamu.

Katika ripoti yake mpya, shirika la Human Rights Watch limesema, hali ya haki za binadamu katika nchi za Bahrain na Saudi Arabia ni ya kusikitisha mno na kuongeza kuwa, siasa za kushadidia Uarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi, daima zimekuwa zikienda sambamba na kukandamizwa wapinzani wake, kutiwa mbaroni na kuteswa, huku vyombo vya dola na vikosi vya usalama vya nchi hizo vikiwakandamiza kikatili wapinzani wa tawala zilizoko madarakani.

 

Shirika la Human Rights Watch limesisitiza pia kuwa, kutiwa mbaroni mawakili na wanasheria pamoja na waandishi wa habari katika nchi hizo za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi, kunazifanya nchi hizo kuwa na viwango vya juu vya ukandamizaji na kukosa viwango hata vya chini kabisa vya haki za binadamu. 

Tags