Bunge la Israel lautupa muswada wa kupiga marufuku Adhana
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i20959-bunge_la_israel_lautupa_muswada_wa_kupiga_marufuku_adhana
Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel Knesset leo Jumatano limeutupilia mbali muswada wa kupiga marufuku adhana katika mji mtakatifu wa Quds na maeneo mengine ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 07, 2016 12:15 UTC
  • Bunge la Israel lautupa muswada wa kupiga marufuku Adhana

Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel Knesset leo Jumatano limeutupilia mbali muswada wa kupiga marufuku adhana katika mji mtakatifu wa Quds na maeneo mengine ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

Muswada huo ulikuwa upigiwe kura leo Jumatano ndani ya bunge hilo lakini kanali ya 10 ya televisheni ya utawala wa Kizayuni imetangaza kuwa, muswada huo umekataliwa kutokana na makosa yaliyomo kwenye rasimu yake.

Moti Yogev wa chama cha al Beyt al Yahudi pamoja na Robert Ilatov wa chama cha Yisrael Beiteinu, ndio waliowasilisha muswada huo katika bunge hilo.

Awali muswada huo ulikuwa upigiwe kura Jumanne ya Novemba 22, lakini uliakhirishwa hadi Jumatano iliyopita ya tarehe Mosi Disemba, ambapo  kutokana na sababu mbalimbali uliakhirishwa tena hadi Disemba 5 na leo Jumatano kanali ya kumi ya televisheni ya Israel imetangaza kuwa, Bunge la utawala huo limeupiga teke muswada huo kutokana na makosa yaliyomo kwenye rasimu yake.

 

Naye David Lawi, kuhani wa utawala wa Kizayuni amegusia kwamba sheria ya kupiga marufuku adhana katika misikiti ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu haina uhalali wowote wa kidini na kisheria na kusema kuwa, kuna juhudi kubwa zinafanyika za kuuzuia utawala wa Kizayuni kupitisha sheria kama hiyo.

Wakazi wa mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas nao waliamua kupanda juu ya mapaa ya nyumba zao na kusoma adhana kwa sauti kubwa kama njia ya kuonesha kukasirishwa kwao na njama za serikali ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kupiga marufuku adhana misikitini.