Maelfu ya watu watiwa mbaroni Saudi Arabia kwa tuhuma za ugaidi
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imetangaza habari ya kutiwa nguvuni maelfu ya watu nchini humo kwa tuhuma za kuwa na mahusiano na makundi ya kigaidi.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imearifu kuwa jumla ya watu 5167 wanashikiliwa katika jela za ofisi ya uchunguzi na ya mwendesha mashtaka mkuu kwa tuhuma za kujihusisha na masuala ya ugaidi. Hii ni katika hali ambayo hukumu imetolewa kwa baadhi ya watuhumiwa ambao imeelezwa kuwa wametumikia baadhi ya adhabu zao; huku wengine wakiendelea kuhukumiwa na kuchunguzwa. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imeongeza kuwa, miongoni mwa watu waliotiwa nguvuni kwa tuhuma za ugaidi wako pia raia wa Misri, Pakistan, Yemen na Syria mbali na raia wa Saudia.
Saudi Arabia ambayo yenyewe inayaunga mkono makundi ya kigaidi imekuwa ikiwatia mbaroni watu nchini humo kwa kisingizio cha kujihusisha na vitendo vya kigaidi. Saudia na Qatar ni nchi zinazoyaunga mkono kifedha makundi tofauti ya kigaidi yakiwemo makundi ya Daesh na Jabhatul Nusra katika eneo hili. Kwa kufanya hivyo nchi hizo zinajaribu kujidhihirisha kuwa zinaendesha mapambano ya kweli dhidi ya ugaidi.