Mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu Bahrain aachiwa huru
Nabil Rajab, mwanaharakati mtajika wa kutetea haki za binadamu nchini Bahrain ambaye amezuiliwa kwa miezi kadhaa na polisi ya nchi hiyo ameachiwa huru kufuatia mashinikizo ya ndani na nje ya nchi.
Jalila Sayed, wakili wa mwanaharakati huyo amesema mteja wake ameachiwa huru leo Jumatano kwa misingi ya hali yake ya afya na kwamba, atafikishwa mahakamani Januari 23 kusikiliza kesi dhidi yake.
Amefafanua kuwa, Nabil Rajab mwenye umri wa miaka 52 ana ugonjwa wa moyo na kubainisha kuwa amedhoofika kiafya kutokana na msongo wa mawazo kwa kuzuiliwa kwa kipindi kirefu chini ya mazingira magumu.
Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa uliutaka utawala wa Aal Khalifa umwachie huru haraka na bila ya masharti yoyote mwanaharakati huyo wa kutetea haki za binadamu nchini Bahrain.
Liz Throssel, msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa wana wasiwasi mkubwa mno na mwenendo wa uendeshaji kesi inayomkabili Rajab na kwamba alikamatwa kwa sababu ya kutumia haki yake ya kutoa maoni. Kadhalika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limewahi kukosoa vikali kuendelea kuzuiliwa kinyume cha sheria mwanaharakati huyo likisisitiza kuwa haki yake ya msingi ya kujieleza imekanyagwa.
Nabil Rajab alitiwa nguvuni tarehe 13 Juni mwaka huu kutokana na kuukosoa utawala wa Bahrain wa Aal Khalifa kwa kushiriki kwenye uvamizi ulioongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen. Endapo atapatikana na hatia kwa sababu ya tuhuma hizo anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.