Kuhamishiwa Quds ubalozi wa US, mstari mwekundu kwa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i22987-kuhamishiwa_quds_ubalozi_wa_us_mstari_mwekundu_kwa_palestina
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas amemuonya Rais mteule wa Marekani Donald Trump kuhusu pendekezo lake la kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 07, 2017 03:42 UTC
  • Kuhamishiwa Quds ubalozi wa US, mstari mwekundu kwa Palestina

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas amemuonya Rais mteule wa Marekani Donald Trump kuhusu pendekezo lake la kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds Tukufu.

Abbas aliyasema hayo jana katika mji wa Bethlehem, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuongeza kuwa, kutekelezwa mpango huo kutakuwa ni kuhujumu uhuru wa taifa la Palestina.

Ameonya kuwa, iwapo Marekani itatekeleza azma hiyo ya kubadilisha hali ya Quds Tukufu itakuwa imekanyaga mstari mwekundu, jambo ambalo Wapalestina hawatalikubali.

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump

Kufuatia hatua ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina mwezi uliopita, Trump alisisitizia udharura wa ubalozi wa nchi hiyo ulioko Tel Aviv uhamishiwe haraka mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu.

Mwezi uliopita, Khatibu wa Sala ya Ijumaa katika msikiti mtukufu wa Al-Aqsa, Palestina inayokaliwa kwa mabavu alisema, kuhamishiwa Baitul Muqaddas ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv na kuitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa utawala bandia wa Israel ni sawa na kutangaza vita na Wapalestina na Waislamu duniani kote.

Aidha Saeb Erekat Katibu Mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO hivi karibuni alisema kuhusiana na mpango huo kuwa, hatua kama hiyo itapelekea kuangamia mpango wa kile kinachotajwa kuwa ni mazungumzo ya amani ya Palestina na Israel.