Kuendelea ukandamizaji wa utawala wa Aal-Khalifa mwaka 2017 huko Bahrain
Kutolewa hukumu ya adhabu ya kifo, unyang'aji wa uraia uliofanywa na mahakama na kadhalika kupiga marufuku vikao na majlisi za maombelezo kwa ajili ya vijana wanaouawa shahidi nchini Bahrain ni ishara ya kuendelea siasa za ukandamizaji za utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya raia wa nchi hiyo mwaka huu wa 2017.
Mwaka 2017 umeanza na ukandamizaji wa hali ya juu unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya raia wake. Utawala wa kifalme wa nchi hiyo unatumia njia tofauti za ukandamizaji dhidi ya wapinzani wake na wanaokumbwa na ukandamizaji huo ni raia wa kawaida, viongozi wa dini na wanaharakati wa kisiasa.
Katika mwendelezo wa utoaji hukumu zisizo za kiadilifu na ukandamizaji dhidi ya wapinzani, Jumatano ya jana ya tarehe 29 Machi mahakama ya utawala huo iliwahukumu raia wawili adhabu ya kifo kwa tuhuma za mauaji ya polisi wawili. Mwezi Januari mwaka huu pia mahakama hiyo ilitoa hukumu kama hiyo dhidi ya raia watatu wa Bahrain kwa tuhuma za kile kilichosemwa kuwa ni kuhusika kwao katika tukio la kigaidi la mwezi Machi mwaka 2014.
Hukumu ya kufutiwa uraia ambazo zimekuwa zikitolewa na mahakama za Bahrain katika kipindi cha miaka sita iliyopita dhidi ya raia, wanaharakati wa kisiasa na hata viongozi wa kidini kwa mara nyingine tena ilitolewa hapo jana dhidi ya raia wanane wa nchi hiyo kwa tuhuma bandia za kuhusika katika mauaji ya polisi wawili. Moja ya hukumu hizo za kufutiwa uraia zilizowahi kutolewa na mahakama za utawala wa kidikteta wa Aal-Khalifa na kupingwa ndani na nje ya nchi hiyo ni ile ya kumfutia uraia Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa kiroho wa wananchi wa Bahrain, hukumu ambayo ilitolewa mwezi Juni mwaka jana.
Aidha hukumu za vifungo vya muda mrefu dhidi ya raia, wanaharakati na viongozi wa dini ni sehemu nyingine ya ukandamizaji uliokithiri nchini Bahrain, ambapo mwaka huu pia umeendelea kushuhudiwa. Katika uwanja huo Mahakama ya Rufaa ya Bahrain Jumatano ya jana ya tarehe 29 Machi, ilimhukumu kifungo cha miaka 10 jela Sheikh Hassan Isa ambaye ni miongoni mwa maulama wakubwa wa chama cha Kiislamu na kitaifa cha al-Wefaq katika faili la mauaji ya polisi wawili.
Utawala wa kifalme wa Bahrain unaendelea kukiuka waziwazi haki za kijamii za raia wake ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku vikao na majlisi za maombolezo kwa ajili ya kijana Mustafa Hamdan, aliyepigwa risasi mwezi Januari mwaka huu katika maandamano ya amani akafariki dunia siku ya Ijumaa iliyopita ya tarehe 24 Machi kutokana na majeraha makubwa. Kisingizio kinachotolewa na mahakama ya Aal-Khalifa kwa ajili ya kutoa hukumu hizo dhidi ya wapinzani wake ni kuhusika katika mauaji ya polisi wawili.
Utawala wa nchi hiyo unawahami na kuwashajiisha polisi kuwashambulia vikali waandamanaji na kutumia mabavu na ukatili dhidi ya raia, suala ambalo linabainisha kwamba ukandamizaji nchini Bahrain unafanyika kwa malengo maalumu kuanzia ngazi ya juu kwenda chini. Aidha utawala wa kidikteta wa Bahrain unawahami polisi wanaofanya ukatili dhidi ya raia katika hali ambayo akthari ya polisi wa nchi hiyo ni wageni ambao Aal-Khalifa waliwapatia uraia wa nchi hiyo.
Mienendo ya utawala wa Bahrain inaonyesha kwamba, mwaka huu wa 2017 utakuwa mwaka ambao kutashuhudiwa sana ukandamizaji na ukatili dhidi ya raia wa nchi hiyo muitifaki mkubwa wa madola ya Magharibi na Saudi Arabia.