EU: Hatutohamishia balozi zetu Quds tukufu kutoka Tel Aviv
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27290-eu_hatutohamishia_balozi_zetu_quds_tukufu_kutoka_tel_aviv
Katika hali ambayo Marekani imezungumzia mpango wa kuhamishia ubalozi wake ulioko Israel kutoka Tel Aviv na kuupeleka katika mji wa Quds tukufu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Umoja wa Ulaya umesema nchi wanachama wake hazitofuata sera hizo za Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2017 11:21 UTC
  • EU: Hatutohamishia balozi zetu Quds tukufu kutoka Tel Aviv

Katika hali ambayo Marekani imezungumzia mpango wa kuhamishia ubalozi wake ulioko Israel kutoka Tel Aviv na kuupeleka katika mji wa Quds tukufu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Umoja wa Ulaya umesema nchi wanachama wake hazitofuata sera hizo za Washington.

Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje za Umoja wa Ulaya amesema kuwa, nchi wanachama wa EU hazina mpango wowote wa kuzihamishia balozi zake Quds tukufu kutoka Tel Aviv.

Shirika rasmi la habari la Kuwait KUNA limemnukuu Mogherini akisema kuwa: "Msimamo wetu ni sawa na ule wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu unaosisitiza kuwa, kuhamishiwa balozi Quds tukufu kutavuruga zaidi kile kinachoitwa mchakato wa kuundwa nchi mbili, kama njia ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa muda mrefu Mashariki ya Kati."

Ahmad Abulgheit, Katibu Mkuu wa Arab League

Mogherini ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari huko Luxemberg, akiwa pamoja na Ahmad Abul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amesema kuwa kitendo cha kuuhamishia ubalozi wa Marekani huko Baitul Muqaddas kutakuwa na taathira hasi kwa ufumbuzi wa kadhia ya Palestina. 

Huko nyuma Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO ilitahadharisha kuhusu azma ya Marekani ya kuuondoa ubalozi wake mjini Tel Aviv na kuuhamishia katika mji wa Baytul Muqaddas na kusisitiza kuwa, hatua hiyo ni hatari na itasababisha maafa makubwa. Kadhalika Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas hivi karibuni alimwandikia barua Rais wa Marekani Donald Trump na kumuonya juu ya taathira hasi za pendekezo lake la kuuhamishia ubalozi wa Marekani Quds tukufu.