Apr 09, 2017 02:38 UTC
  • Maandamano ya wananchi wa Syria ya kulaani jinai za Marekani

Wananchi wa Syria wamefanya maandamano katika mitaa ya Damascus mji mkuu wa nchi hiyo kulaani mashambulizi ya Marekani katika kituo cha jeshi la anga cha nchi hiyo.

Katika maandamano hayo, wananchi wa Syria wametaka kutolewa majibu makali dhidi ya uchokozi huo wa Marekani. Mmoja wa washiriki wa maandamano hayo ameeleza kuwa shambulio la Marekani dhidi ya kituo  cha jeshi la anga la Syria ni jinai ya kivita na kwamba wananchi wa Syria hawayaafiki mashambulizi hayo kivyovyote vile hasa kwa kuzingatia kuwa wanajeshi wa Syria waliouawa kwenye hujuma hiyo ni raia wa nchi hiyo. Sambamba na kufanyika maandamano ya wananchi ya kulaani na kupinga shambulizi la kijeshi la Marekani huko Syria, serikali ya Damascus pia imesisitiza wazi kwamba, uvamizi uliofanywa na Marekani nchini humo umezidisha azma na nia ya nchi hiyo ya kuwashambulia magaidi mamluki na kuendelea kuwaaangamiza katika kila eneo walipo ndani ya ardhi ya Syria na itaendelea pia kufuatilia kwa hisia kubwa harakati za magaidi hao. 

Juzi alifajiri Marekani ilivurumisha makombora 59  kutokea katika meli zake mbili za kivita katika bahari ya Mediterania na kukishambulia kituo cha jeshi la anga la Syria katika eneo la Shayrat katika mkoa wa Homs na kuuwa watu tisa wakiwemo watoto wanne na kujeruhi wengine kadhaa. Marekani imefanya mashambulizi hayo kwa madai ya kujibu shambulio eti la kemikali linalodaiwa kufanywa na serikali ya Syria katika mkoa wa Idlib Jumanne iliyopita. Mashambulizi hayo ya anga ya Marekani yamesababisha hasara na maafa makubwa kwa nyumba za vijiji vya al Hamrat, al Shayrat na al Manzur ambavyo viko karibu na kituo cha jeshi la anga huko al Shayrat.

 

Meli ya kivita ya Marekani iliyovurumisha makombora katika kituo cha anga Syria 

Kushtadi harakati za ungiliaji kati za Marekani huko Syria ni ukiukaji mkubwa wa mamlaka ya kujitawala nchi hiyo. Kitendo hicho kinakinzana waziwazi na sheria za kimataifa. Mbali na kuua baadhi ya wanajeshi wa Syria wanaoendesha mapambano dhidi ya magaidi, mashambulizi hayo ya Marekani yameua pia mamia ya raia wa nchi hiyo sambamba na kubomoa nyumba za raia na majengo ya serikali.

Marekani imefanya jinai hizo  lengo likiwa ni kushadidisha machafuko, kufanya uharibifu mkubwa zaidi na kuyatia moyo magenge ya kigaidi huko Syria. Mashambulizi hayo yana mfungamano wa moja kwa moja na hujuma na mashambulizi yanayofanywa na makundi ya kigaidi kama Daesh, Jabhatul Nusra na baadhi ya watu na makundi yenye mfungamano nayo. Ni wazi kuwa Marekani na magaidi mamluki wanafanya jinai kwa pamoja ili kupitia kushadidisha mauaji ya wananchi huko Syria. Katika hatua zake za kijeshi za moja kwa moja ndani ya ardhi ya Syria na au kupitia muungano eti wa kupambana na Daesh, Marekani katika miaka ya hivi karibuni imekanyaga haki ya kujitawala ardhi yote ya Syria kwa njia mbalimbali. Uvamizi wote huo unafanyika bila ya idhini ya Umoja wa Marekani wala ombi kutoka kwa serikali ya Syria. 

Ndege ya kivita ya Marekani inayouwa raia huko Syria aina ya F-16  

Hii ni katika hali ambayo hatua za uingiliaji kati na za  upande mmoja za Marekani huko Syria bila ya kibali cha Umoja wa Mataifa zimeongezeka katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Donald Trump. Hapana shaka kuwa hatua yoyote ya kutumia mabavu na ya kifedhuli ambayo iko nje ya sheria za kimataifa ambayo haiheshimu mamlaka ya kujitawala nchi nyingine, inahesabiwa kuwa ni ukiukaji wa moja kwa moja wa haki ya kujitawala kila nchi. Hakuna kisingizio kinachoweza kuhalalisha na kufunika ukiukaji huo wa mamlaka ya kujitawala nchi ya Syria na mauaji ya raia wa nchi hiyo yanayofanywa na Marekani pamoja na jinai nyingine chungu nzima za kivita za nchi hiyo huko Syria. 

Radiamali kubwa zilizotolewa na viongozi na wananchi wa Syria pamoja na fikra za walio wengi duniani katika miezi ya hivi karibuni kutokana na chokochoko za Marekani katika eneo hili hususan hatua zake za kukanyaga kila siku mamlaka ya kujitawala nchi ya Syria, zinadhihirisha namna siasa za nje za Washington zinazozusha mivutano, zinavyokabiliwa na upinzani mkubwa kila uchao. Hapana shaka kuwa hatua za Washington zimeifanya migogoro kuwa migumu zaidi na kuongeza hatari ya ukosefu wa amani katika eneo la Mashariki ya Kati.

Tags