Wapalestina 400 wakamatwa kwa kutumia Facebook kupinga Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i27862-wapalestina_400_wakamatwa_kwa_kutumia_facebook_kupinga_israel
Utawala wa Kizayuni wa Israel umewakamata Wapalestina 400 kwa sababu ya kuandika maneno yaliyo dhidi ya utawala huo katika mtandao wa kijamii wa Facebook.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 16, 2017 22:24 UTC
  • Wapalestina 400 wakamatwa kwa kutumia Facebook kupinga Israel

Utawala wa Kizayuni wa Israel umewakamata Wapalestina 400 kwa sababu ya kuandika maneno yaliyo dhidi ya utawala huo katika mtandao wa kijamii wa Facebook.

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeandika kuwa, kutokana na ugumu wa kubaini wanaotekeleza oparesheni  za kuwaangamiza Wazayuni katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), hivi sasa jeshi la Israel limeamua kudhibiti mitandao ya kijamii. Kwa msingi huo Wapalestina wanaoandika au kueneza picha na taswira za video dhidi ya Israel sasa wanasakwa kwa msaada wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kukamatwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utawala haramu wa Israel umewakamata Wapalestina 400 kwa kuhusika na harakati dhidi ya utawala huo katika Facebook. Waliokamatwa pia wanatuhumiwa kuhusika na njama za kutekeleza oparesheni dhidi ya Israel.

Wanajeshi wa Israel wakiuhujumu Msikiti wa Al Aqsa

Utawala wa Kizayuni wa Israel umezidisha jinai dhidi ya Wapalestina wakiwemo watoto miongoni mwao. Utawala huo umekuwa ukihujumu maeneo matukufu ya Kiislamu hasa Msikiti wa Al Aqsa ambapo utawala huo unapanga kuugawa msikiti huo kwa eneo na zama. Njama hiyo ilianza Oktoba 2015 na kuibua Intifadha au mwamko wa tatu wa Wapalestina na tangu wakati huo hadi sasa, Wapalestina zaidi ya 300 wameuliwa shahidi na wanajeshi wa Israel na wengine wengi kujeruhiwa.