Nchi za Kiislamu zatakiwa kuwaunga mkono wafungwa wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28300-nchi_za_kiislamu_zatakiwa_kuwaunga_mkono_wafungwa_wa_palestina
Balozi wa Palestina mjini Tehran amesema Palestina itaweza kusaidika iwapo kutakuwa na umoja katika ulimwengu wa Kiislamu huku akitoa wito kwa nchi za Kiislamu kuwaunga mkono wafungwa wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 27, 2017 02:46 UTC
  • Nchi za Kiislamu zatakiwa kuwaunga mkono wafungwa wa Palestina

Balozi wa Palestina mjini Tehran amesema Palestina itaweza kusaidika iwapo kutakuwa na umoja katika ulimwengu wa Kiislamu huku akitoa wito kwa nchi za Kiislamu kuwaunga mkono wafungwa wa Palestina.

Akizungumza Jumatano mjini Tehran kwa munasaba wa Siku ya Wafungwa wa Palestina, Balozi Salah Zawawi Balozi wa Palestina mjini Tehran ameashiria kususia kula chakula wafungwa 1,500 wa Palestina ambao wanashikiliwa katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: "Nchi za Kiislamu zinapaswa kutumia kila mbinu iwe ni katika vyombo vya habari au taasizi za kielimu na kimataifa kuangazia kadhia ya wafungwa wa Palestina na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu."

Balozi Zawawi amesema nchi za Magharibi ndizo zilizowachochea Mayahudi kuhamia katika ardhi za Palestina ili kuundwe dola bandia la Israel na hivyo kutenganisha nchi za Kiislamu katika mabara ya Asia na Afrika.

Msikiti wa Al Aqsa unaokaliwa kwa mabavu na Israel

Mwanadiplomasia huyo wa Palestina ameashiria vita vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni ili kughusubu kikamilifu ardhi zote za Palestina na baadhi ya nchi za Kiarabu na kusema: "Utawala wa Kizayuni unalenga kuunda Israel Kubwa kutoka Mto Nile hadi Mto Furat na lengo hilo linafuatiliwa kwa msaada wa Uzayuni wa kimataifa na Marekani." Balozi Zawawi pia ameashiria lengo la Marekani katika kutoa pigo kwa ulimwengu wa Kiislamu na kusema: "Iraq na Afghanistan zimevamiwa na Marekani na sambamba na hilo magaidi wamepewa kila aina ya silaha huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikipingwa vikali, lengo likiwa ni kuudhoofisha Ulimwengu wa Kiislamu."