Arab League yautaka Msalaba Mwekundu kutetea wafungwa wa Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28318-arab_league_yautaka_msalaba_mwekundu_kutetea_wafungwa_wa_palestina
Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimelitaka shirika la Msalama Mwekundu kuwaunga mkono na kusimama na wafungwa wa Palestina sambamba na kusaidia kukomeshwa jinai dhidi yao wanazofanyiwa na utawala haramu wa Israe.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 27, 2017 08:14 UTC
  • Arab League yautaka Msalaba Mwekundu kutetea wafungwa wa Palestina

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimelitaka shirika la Msalama Mwekundu kuwaunga mkono na kusimama na wafungwa wa Palestina sambamba na kusaidia kukomeshwa jinai dhidi yao wanazofanyiwa na utawala haramu wa Israe.

Ahmed Aboul Gheit, Katibu Mkuu wa Arab League amemuandikia barua Peter Maurer, Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu akiitaka jumuiya hiyo iingilie kati na kukomesha ukandamizaji na mateso dhidi ya wafungwa wa Kipalestina katika jela za kutisha za utawala huo wa Kizayuni.

Kadhalika barua hiyo ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imeliiomba shirika la Msalaba Mwekundu kuwashurutisha watawala wa Israel kuangalia maslahi ya wafungwa waliosusia kula wa Kipalestina, kwa mujibu wa miongozo na viwango vya sheria ya kimataifa ya kibinadamu. 

Wafungwa wa Kipalestina

Akizungumza jana Jumatano hapa nchini, kwa mnasaba wa Siku ya Wafungwa wa Palestina, Salah Zawawi, Balozi wa Palestina mjini Tehran aliashiria kususia kula chakula wafungwa 1,500 wa Palestina ambao wanashikiliwa katika jela za utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: "Nchi za Kiislamu zinapaswa kutumia kila mbinu iwe ni katika vyombo vya habari au taasizi za kielimu na kimataifa kuangazia kadhia ya wafungwa wa Palestina na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu."

Mgomo wa kususia kula Wapalestina zaidi ya 1,500 wakiongozwa na Marwan Al-Barghuthi ambaye anatumikia kifungo cha maisha jela ulianza tarehe 17 Aprili kwa kaulimbiu ya "Uhuru na Heshima" katika magereza yote ya utawala wa Kizayuni.