Israel yaanza tena ujenzi wa ukuta wa kibaguzi Ukingo wa Magharibi
Utawala haramu wa Israel umeanza tena ujenzi tata wa ukuta wa kibaguzi unaotenganisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mji wa Beit Lahm.
Ukuta huo unatazamwa kama kielekezo cha sera za ukandamizaji zinazotekelezwa na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Wanajeshi wa Israel wameweka seng'enge yenye urefu wa mita nne katika eneo la Ein Jwaizeh kaskazini magharibi mwa kijiji cha al-Walaja na hivyo kukizingira kikamilifu. Hassan Brijiyeh wa kamati ya kupinga Ukuta wa Kibaguzi na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Bait Lahm amesema ujenzi wa ukuta huo ni ukiukwaji wa haki za Wapalestina kwani utaweka vizingti katika uwezo wao wa kufika katika ardhi zao na pia kuwazuia kupata huduma muhimu na kuwatembelea jamaa zao walio katika upande wa pili wa ukuta.
Utawala ghasibu wa Israel ulianza kujenga ukuta huo wa kibaguzi mwaka 2002 na hadi sasa umekamilisha asilimia 75 ya ukuta huo ambao utakapokamilika utakuwa na urefu wa karibu kilomita 700.
Ujenzi wa ukuta huo ulianza kupingwa na jamii ya kimataifa tangu awamu za kwanza wa ujenzi wake. Mahakama ya Kimataifa ya The Hague huko Uholanzi mwaka 2004 ilitoa hukumu ikiutaja ujenzi huo kuwa ni kinyume cha sheria na ikatoa amri ya kuvunjwa na kutolewa fidia kwa wananchi wa Palestina. Hata hivyo nchi za Magharibi si tu kwamba hazijatekeleza hukumu hiyo ya mahakama ya kimatafa bali zinaendelea kuusaidia utawala ghasibu wa Israel katika ujenzi wa ukuta huo wa kibaguzi katika ardhi za Palestina.