Makumi wauawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu Kabul
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28590-makumi_wauawa_na_kujeruhiwa_katika_mripuko_wa_bomu_kabul
Watu 33 wameuawa na kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu ulioutikisa mji wa Kabul karibu na ubalozi wa Marekani nchini Afghanistan mapema leo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 03, 2017 03:17 UTC
  • Makumi wauawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu Kabul

Watu 33 wameuawa na kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu ulioutikisa mji wa Kabul karibu na ubalozi wa Marekani nchini Afghanistan mapema leo.

Habari zinasema kuwa, miongoni mwa watu waliouawa katika shambulizi hilo la bomu ni askari watatu wa Marekani na kwamba hujuma hiyo ililenga msafara wa magari ya Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO). 

Habari zaidi zinasema kuwa, kwa akali watu wanane wameuawa huku wengine zaidi ya 25 wakijeruhiwa, katika hujuma hiyo iliyotokea katika eneo la Macroyan mjini Kabul. 

Haadi tunaenda mitamboni, hakuna kundi lililokuwa limetangaza kuhusika na shambulizi hilo. Hata hivyo hivi karibuni, kundi la kigaidi la Taliban lilitangaza kuwa litashadidisha vita dhidi ya maafisa usalama wa nchi hiyo na vikosi vamizi, katika operesheni waliyoipa jina la "Mashambulizi ya Machipuo".

Shambulizi dhidi ya magari ya NATO

Mwezi uliopita wa Aprili, watu 28 waliuawa huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa katika shambulizi jingine la kigaidi lililotokea karibu na ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Shambulizi hilo lilifanyika siku chache baada ya jeshi la Marekani kushambulia Afghanistan kwa kutumia bomu lenye nguvu kubwa zaidi la nchi hiyo lisilo la nyuklia, la GBU-43B maarufu kwa jina la "Mama wa Mabomu Yote".