Khalid Mash'al asisitizia kuendelezwa mapambano ya Wapalestina dhidi ya Israel
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ametangaza kuwa, mapambano na muqawama wa wananchi wa Wapalestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel utaendelea madhali kuna uvamizi na kunaendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina.
Khalid Mash'al amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani na kubainisha kwamba, Hamas ni harakati yenye azma na ambayo iko macho katika mahesabu ya Mashariki ya Kati na kimataifa kwa ujumla.
Khalid Mash'al amebainisha kwamba, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS inaheshimu demokrasia huko Palestina na inasisitizia wajibu wa kuheshimiwa matokeo ya uchaguzi.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesema katika sehemu nyingine ya mahojiano yake hayo kwamba, harakati hiyo si yenye kutumia mabavu bali inachokifanya nai kuendesha mapambano na muqawama dhidi ya uvamizi na ukaliaji mabavu wa Israel kwa ardhi za Palestina.
Mash'al amesisitiza kuwa, madhali uvamizi na ukaliaji mabavu pamoja na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ungali unaendelea katika ardhi za Palestina, basi muqawama nao dhidi ya utawala vamizi wa Israel utaendelea kushuhudiwa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina inayoongozwa na Mahmoud Abbas imeendelea kukosolewa wanaharakati mbalimbali wa Palestina kutokana na kuweko ushirikiano wa kiusalama baina yake na utawala wa Kizayuni wa Israel, ushirikiano ambao unatajwa kuwa kikwazo cha kufikiwa malengo ya Wapalestina.