Wabahrain waandamana nchi nzima huku kesi ya Sheikh Qassim ikiskizwa leo
Wananchi wa Bahrain wamejitokeza mabarabarani kushiriki maandamano ya nchi nzima leo Jumapili, siku ya kusikilizwa kesi ya Ayatullah Sheikh Isa Qassim, mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Wananchi wamejitokeza kwa wingi kushiriki maandamano hayo ya amani, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na wanazuoni wa Kiislamu nchini Bahrain ambao hivi karibuni walitoa wito kwa wananchi kupinga hukumu yoyote ya mahakama dhidi ya mwanazuoni huyo mtajika.
Maafisa usalama nchini Bahrain tangu jana usiku wamewekwa katika hali ya tahadhari katika pembe mbali mbali za nchi.
Maandamano haya yanafanyika siku tatu baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Bahrain na kimataifa kuziandikia barua Marekani, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya yakizitaka ziishinikize serikali ya Manama kukomesha jinai zake dhidi ya Sheikh Issa Qassim, mwanazuoni mashuhuri wa ngazi ya juu wa nchi hiyo ambaye alivuliwa uraia wa Bahrain Juni 20 mwaka jana 2016.
Vyombo vya mahakama vya utawala dhalimu wa Aal-Khalifa nchini Bahrain vinatazamiwa kutoa hukumu dhidi ya Sheikh Qassim hii leo, ambapo mwanazuoni huyo anakabiliwa na tuhuma bandia kwamba amekuwa akieneza chuki za kimadhehebu miongoni mwa watu wa Bahrain mbali na kuchochea machafuko na kuhatarisha usalama wa taifa. Kadhalika wanazuoni wawili waliokuwa wakifanya kazi katika ofisi ya Ayatullah Qassim, ambao ni Sheikh Hussein Mahrous na Mirza al-Dirazi, wanatazamiwa kupandishwa kizimbani hii leo wakikabiliwa na tuhuma kama za Sheikh Qassim.
Tokea tarehe 14 Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati za mwamko wa Kiislamu dhidi ya ukandamizaji na mbinyo wa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi.