Kuendelea mauaji dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Saudi Arabia
Vyombo vya habari vimeripoti habari ya kuuawa kijana mmoja nchini Saudi Arabia kufuatia hujuma ya jeshi la utawala wa Aal Saud katika kijiji cha al-Awamiyah mashariki mwa nchi hiyo.
Duru zinazofungamana na wapinzani nchini Saudia zimeripoti kwamba, Wahab Fikri Maayuuf, amekufa shahidi baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi katika eneo hilo la al-Awamiyah. Katika upande mwingine mitandao ya kijamii imeripoti habari ya kuwekwa askari walenga shabaha juu ya majengo huko al-Awamiyah.
Ikiwa ni katika kushadidisha hujuma zao za kijeshi katika kitongoji cha al-Awamiyah, vikosi vya usalama vya Aal Saud vimechukua hatua zenye lengo la kuwazingira Waislamu wa madhehebu ya Shia wa eneo hilo huku vikitumia mabomu na risasi zinazozalisha moto kwa ajili ya kuchoma nyumba za eneo hilo. Katika siku za hivi karibuni kufuatia kushadidi hujuma na mashambulio ya utawala wa Aal Saud katika maeneo ambayo ni ya Mashia mashariki mwa nchi hiyo, mamia ya Waislamu hao wa Kishia wameuawa.
Kuendelea mauaji dhidi ya Waislamu wa Kishia yanayofanywa na utawala wa Aal Saud kumezifanya jinai za familia hiyo zizidi kuonekana. Utawala wa familia ya Aal Saud nchini Saudia badala ya kuchukua hatua zitakazopelekea kupunguza malalamiko na upinzani dhidi yake kwa kuwaridhisha wananchi, umeamua kutumia mkono wa chuma dhidi ya mrengo wa upinzani.
Katika miaka ya hivi karibuni utiaji mbaroni kiholela, mateso, ukandamizaji na kutolewa hukumu zisizo za kiadilifu ni mambo ambayo yameshuhudiwa yakiongezeka mno nchini Saudia, ambapo mauaji dhidi ya Mashia ni kilele cha ukatili wa utawala huo.
Kushadidi ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Kishia si tu kwamba, hakujawa na faida yoyote kwa utawala wa Riyadh bali kumeufanya mgogoro wa ndani nchini humo uzidi kutokota na kushika kasi. Baada ya Saudia kushadidisha vitendo vya ukandamizaji katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ambapo akthari ya wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, kumeibuka malalamiko makubwa katika maeneo hayo na kupelekea kuzuka makabiliano baina ya vikosi vya usalama na raia wa kawaida.
Ushahidi unaonyesha kuwa, maeneo ya mashariki mwa Saudi Arabia yatashuhudia matukio ya kuongezeka hatua za kiusalama katika masaa yajayo na harakati dhidi ya raia. Hata kama ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudia na ukandamizaji wa utawala wa Aal Saud unawahusisha wananchi wote wa nchi hiyo, lakini Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo ndio ambao wamekuwa wakikabiliwa na ukandamizaji mkubwa zaidi ikilinganishwa na matabaka mengine ya wananchi. Watawala wa Saudia wakiwa na mtazamo wa kibaguzi, wamekuwa wakiwahesabu Mashia kama raia wa daraja la pili nchini humo. Ubaguzi huo umewafanya Mashia wanyimwe haki zao nyingi. Waislamu wa Kishia wanaunda asilimia 10 hadi 15 ya raia wote wa Saudia na wanapatikana zaidi katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.
Huku raia wa nchi hiyo wakikabiliwa na ukandamizaji, kupokonywa uhuru wa kutoa maoni na kunyimwa haki zao, watawala wa nchi hiyo wamekuwa wakitumia pato la nchi hiyo na suhula nyingine muhimu kwa ajili ya kueneza fikra potovu za Kiwahabi. Takwimu zinaonyesha kuwa, Saudia inatumia fedha nyingi mno kwa ajili ya kueneza fikra potovu za Kiwahabi ambazo kimsingi zina mizizi ya itikadi ya ugaidi na utakfiri. Hivi karibuni Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Marekani lilifichua kwamba, Saudia imetumia dola bilioni moja kwa ajili ya kueneza fikra za Kiwahabi duniani.
Kwa kuzingatia kwamba, utawala wa Saudia ni tegemezi, miamala yake pia ni ya karne za kati. Kwa hakika muamala usio wa kibinadamu wa Aal Saud dhidi ya wapinzani na matabaka ya waliowachache wa nchi hjiyo unabainisha wazi juu ya kuweko miamala ya kimakundi na kibaguzi katika dhati ya utawala huo ambao ni dhihirisho la hatua na vitendo vya utawala haramu wa Israel.
Ukweli wa mambo ni kuwa, utawala wa Saudia hauna mpaka wowote katika ukandamizaji ambapo kwa kuwanyonga wapinzani, kuwahukumu jela vifungo vya miaka mingi na kubomoa maeneo na makazi yao umewanyima haki ya kuishi. Hii ni katika hali ambayo, kuendelea hasira na malalamiko ya wananchi wa Saudia dhidi ya siasa za kuhodhi mambo za Aal Saud, utumiaji mabavu na mauaji dhidi ya matabaka mbalimbali ya wananchi wa nchi hiyo hususan wafuasi wa madhehebu ya Shia kumepelekea kupanuka wigo wa malalamiko dhidi ya watawala hao katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hususan mashariki mwa nchi; jambo ambalo linaonyesha kusimama kidete na kutotetereka harakari ya malalamiko ya wananchi dhidi ya utawala wa kidikteta wa Aal Saud.